Rais wa Marekani Donald Trump, amesema kuwa bado “hafahamu cha kuamini” kufuatia majaribio mawili ya kumuua, yaliyotokea wakati wa kampeni yake mwaka jana.
Katika mahojiano yake na chombo cha habari cha Fox, kilichorushwa siku ya Jumatano, Trump amesema kuwa bado hajapata maelezo sahihi kutoka idara ya ulinzi wa viongozi wala FBI kuhusiana na matukio hayo.
"Niwe tu mkweli, sijui niamini nini kwa sasa, kwani sijaambiwa lolote," alisema Trump.
“Tunao watu wawili waaminifu wenye kuongoza mashirika hayo. Ningetamani kusikia watasema nini. Hata kama hakijawekwa hadharani. Nami natakiwa kukisikiliza,” aliongeza.
Julai mwaka jana, mtu mwenye silaha alijaribu kumuua Trump katika kampeni yake jijini Pennsylvania, ambapo alifanikiwa kumjeruhi kiongozi huyo kwenye eneo la sikio.
Hata hivyo, mtu huyo aliuwawa na idara ya ulinzi wa viongozi, muda mfupi baada ya tukio hilo.