Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa Israel inashirikiana na Marekani kutambua nchi ambazo zinaweza "kuwapa Wapalestina mustakabali mwema," alipokutana na Rais wa Marekani Donald Trump katika Ikulu ya White House.
"Israel inashirikiana na Marekani kutafuta nchi ambazo zitawapa Wapalestina maisha bora ya baadaye," Netanyahu aliwaambia waandishi wa habari mwanzoni mwa mkutano huo siku ya Jumatatu.
Kiongozi huyo wa Israel ameongeza kuwa amani inaweza kupatikana na Wapalestina ambao hawataki kuiangamiza Israel, lakini akasisitiza kuwa "nguvu kuu ya usalama daima inabakia mikononi mwetu."
Alipoulizwa iwapo suluhu la mataifa mawili linawezekana, Trump alijibu: "Sijui," na akaelekeza swali hilo kwa Netanyahu, ambaye mara kwa mara amekuwa akipinga utawala wa Palestina.
Trump Nobel
"Baadhi ya watu wanatuomba tuwape Wapalestina dola," Netanyahu alisema.
"Lakini hilo lingekuwa jukwaa la kutuangamiza."
Netanyahu pia alidai kuwa baada ya Oktoba 7, Hamas ilikuwa na taifa katika Israeli, lakini "waliiharibu."
Trump alisema anaamini Hamas iko tayari kukubali kusitisha mapigano.
"Wanataka kukutana na wanataka kuwa na usitishaji huo wa mapigano," alisema.
Netanyahu pia alimkabidhi Trump barua ya kumteua kwa Tuzo ya Amani ya Nobel. "Unastahili," alimwambia rais wa Marekani.
Kujibu, Trump alisema: "kutoka kwako, hii ni ya maana sana."
Mapigano na Iran
Trump alisema anatumai vita kati ya Israel na Iran vimekwisha na akasisitiza kuwa yuko tayari kuondoa vikwazo dhidi ya Tehran "kwa wakati mwafaka."
Amethibitisha kuwa mazungumzo na maafisa wa Iran yamepangwa katika wiki ijayo.
"Tumepanga mazungumzo ya Iran, na wanataka kuzungumza," Trump aliwaambia waandishi wa habari pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya White House.
Mjumbe wa Trump katika Mashariki ya Kati Steve Witkoff alisema mkutano huo utafanyika katika "wiki ijayo au zaidi."
Alipoulizwa kuhusu mashambulio mengine dhidi ya Iran, Trump alisema: "Natumai hatutalazimika kufanya hivyo.
Siwezi kufikiria kutaka kufanya hivyo."
"Natumai yameisha. Ndio, nadhani Iran inataka kukutana. Nadhani wanataka kufanya amani, na ninaiunga mkono," alisema.