SIASA
2 dk kusoma
Jumuiya ya Afrika Mashariki sasa kutumia Kiswahili na Kifaransa
Katika Mkutano wao wa 24 uliofanyika jijini Arusha nchini Tanzania, Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki waliidhinisha lugha hizo mbili, na kufanya Jumuiya hiyo kuwa na jumla ya lugha tatu, ikiwemo na Kiingereza.
Jumuiya ya Afrika Mashariki sasa kutumia Kiswahili na Kifaransa
Makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki / TRT Afrika Swahili
2 Desemba 2024

Lugha za Kiswahili na Kifaransa zimeidhinishwa kuwa lugha rasmi za mawasiliano ndani Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katika Mkutano wao wa 24 uliofanyika jijini Arusha nchini Tanzania, Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki waliidhinisha lugha hizo mbili, na kufanya Jumuiya hiyo kuwa na jumla ya lugha tatu, ikiwemo na Kiingereza.

 Katika taarifa yao, wakuu hao wamependekeza ibara ya 137 ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya hiyo ifanyiwe mabadiliko ili kuzifanya lugha hizo kuwa lugha rasmi ndani ya EAC.

Hapo awali, kifungu hicho kiliitambua lugha ya Kiingereza kuwa lugha rasmi ya mawasiliano ndani ya Jumuiya ya EAC, huku Kiswahili kikitumika kama lugha katika matumizi ya kawaida au ‘lingua franca.’

 Kabla ya uamuzi huo, shughuli nyingi ndani ya makao makuu ya Jumuiya zimekuwa zikiendeshwa kwa lugha ya Kiingereza.

Kwa mfano, shughuli ndani ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) huendeshwa kwa lugha ya Kiingereza.

 Juni 2023, mwakilishi wa DRC ndani ya bunge la EALA, Dorothe Masirika Nganiza, alikumbana na upinzani mkali kutoka kwa wabunge wenzake pale alipojaribu kuwasilisha hoja yake kwa lugha ya Kiswahili ndani ya ukumbi wa bunge hilo.

 Mbunge mwenzake, Gabriel Alaak Garang kutoka Sudan Kusini, alimjulisha mwakilishi huyo kutoka Uganda kuwa lugha rasmi ya mazungumzo ndani ya bunge hilo ilikuwa ni Kiingereza na si vinginevyo.

 Kulingana na Garang, matumizi ya lugha ya Kiswahili ndani ya bunge hilo kwa wakati huo, yangeleta changamoto nyingi na kwamba hata Wasudan Kusini nao wangeomba lugha ya Kiarabu pia itumike ndani ya bunge hilo.

 Kiswahili ni lugha ya taifa katika nchi za Tanzania na Kenya huku Uganda wakitumia Kiingereza kama lugha yao rasmi, huku Kinyarwanda kikitumika kama lugha ya taifa ya Rwanda, Kirundi na Kifaransa nchini Burundi. Kwa upande wa DRC, wao hutumia Kifaransa zaidi kama lugha yao rasmi, japo wanauelewa wa Kiswahili.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us