Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) nchini Kenya imetangaza kuwasimamisha kazi maafisa watano wa kutuo kikuu cha polisi cha Nairobi kufuatia kifo cha Albert Ojwang.
Kupitia taarifa yake katika vyombo vya habari iliyotolewa Jumatatu, Juni 9, NPS ilieleza kuwa walioondolewa ni pamoja na Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS), afisa aliyekuwa zamu usiku wa tukio, afisa wa seli, pamoja na maafisa wote waliokuwa kazini usiku huo.
Inspekta Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja, alisema hatua hiyo inachukuliwa ili kuruhusu uchunguzi huru, na wa haraka na usio na upendeleo kufanyika, chini ya uongozi wa Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA).
Taarifa za kifo cha Ojwang zimeanza kusambaa mwishoni mwa juma na kuibua hisia kali miongoni mwa ndugu, jamaa na marafiki, na Wakenya kwa ujumla, ambao wengi walionyesha hasira zao kupitia mitandao ya kijamii na kulaani kifo cha Ojwang.
Ojwang’ alifariki siku ya Jumapili akiwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Nairobi. Hii ni baada ya kukamatwa Jumamosi alasiri nyumbani kwao Kakot, Kaunti ya Homa Bay, kwa madai ya kuchapisha zenye utata kwenye mtandao wa X.
Baada ya kusafirishwa hadi Nairobi na kuzuiliwa, familia yake ilipofika kituoni kufuatilia kesi hiyo, walikuta tayari amefariki. Kwa mujibu wa polisi, Ojwang alijiua mwenyewe.
Wengi, wanasubiri kuona matokeo ya uchunguzi wa polisi yatakuaje.
Mpaka sasa, bado haijafahamika iwapo, hatua hizi zitatuliza hasira za wananchi au la.