Paul Pogba mwenye umri wa miaka 32 pia alisema kuwa ameanza kuongea na kaka yake Mathias, aliyefungwa mwaka mmoja jela Disemba iliyopita kwa kupanga njama ya kumtapeli dola milioni 19.3 mshindi huyo wa Kombe la Dunia 2018.
Pogba, ambaye alicheza katika timu za Manchester United na Juventus, anatarajia kwamba atasahau miaka mitatu ya dhiki aliyopitia.
Pogba alipata changamoto ya majeraha na kuwa na msimu wa kutokuridhisha jambo lililosababisha aondoke Manchester United 2022. Alirejea tena Juventus, kwa mara ya pili ambapo matatizo yake yaliendelea.
Aligundulika kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni baada ya mechi nchini Italia mwezi Agosti 2023 na kupewa adhabu ya marufuku ya miaka nne kutojihusisha na mpira, ambayo ilipunguzwa hadi miezi 18 baada ya kukata rufaa. Marufuku hiyo ilimalizika mwezi Machi.
“Ilikuwa hali ngumu, ngumu sana,” alisema.
Alisema “anazungumza” na klabu moja, ambapo vyanzo kadhaa vilisema huenda ikawa ni timu ya Ligi Kuu ya Ufaransa Ligue 1 Monaco.
Pogba anasema ana ari “ya kurudi uwanjani, yuko tayari kiakili, yuko tayari kiuwezo, na anasubiri tu”.
Katika kesi ya kutaka kutapeliwa ambapo wanaume sita walitaka kumtapeli Pogba iliwashtua watu wa Ufaransa kwa sababu wahusika walikuwa watu wa karibu na yeye ikiwemo watatu waliokuwa marafiki zake wakiwa wadogo pamoja na kaka yake mwenyewe.