Kuni Poa, nishati safi na salama kwa mazingira
MAZINGIRA
4 dk kusoma
Kuni Poa, nishati safi na salama kwa mazingiraMatumizi ya nishati safi ya kupikia ni ajenda mahususi ambayo imechukua nafasi kubwa katika Sera, Mipango na Mikakati ya Serikali mbalimbali duniani kwa sasa.
Kwa sasa, kampuni ya Hanny G inashirikiana na shule za sekondari zaidi ya 475 nchini Tanzania, magereza 17, vyuo vya elimu 25 na vyuo vikuu viwili./Picha:officialhannyg / Others
7 Aprili 2025

Ulianza kama mradi wa kuzalisha mkaa mbadala, kama njia ya kupunguza ukataji miti kiholela.

Hata hivyo, mradi huo ulilazimika kusitishwa miaka miwili baadaye, kufuatia janga la Uviko 19.

“Tulikuwa tukilenga kutoa huduma kwa wamiliki wa hoteli za kitalii na kwa hakika tulifanikiwa sana tangu tulipoanza mwaka 2016, lakini tulilazimika kusitisha mradi ule baada ya kuzuka kwa janga Uviko 19,” anasema George Lawrence Swai, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa kampuni ya Hanny G Investment, taasisi iliyojikita katika matumizi ya nishati safi, katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Wazo la Kuni Poa

Wakati wa janga la Uviko 19 lilipozidi kupamba moto, Swai na wenzake wakaja na wazo la kutengeneza Kuni Poa.

Kuni hizo, ambazo ni rafiki kwa mazingira hutengenezwa kutoka kwenye mabaki ya miwa, karanga mbichi pamoja na maranda ya mbao.

Kwa mujibu wa Swai, hii ilionekana kuwa dhana mpya kwa Watanzania.

“Kuna waliodhani nimerukwa na akili baada ya kuwapa wazo hilo miaka ile, kwani msisitizo ulikuwa kwenye matumizi ya majiko ya gesi na majiko ya umeme,” Swai anaeleza.

Hata hivyo, kulingana na Swai, Kuni Poa ndio suluhisho sahihi la mazingira kwa sasa, na ndio maana halisi ya nishati jadidifu.

Yenye gharama nafuu na rahisi kutumia

Swai anasisitiza kuwa, Kuni Poa ambazo kwa lugha ya Kiingereza hujulikana kama “briquettes” ni rahisi kutumia na hazina gharama kubwa, ukilinganisha na nyenzo nyingine za nishati.

Kulingana na Swai, ni gharama zaidi kutumia gesi au umeme, ukilinganisha na Kuni Poa.

“Hata ukijaribu kuilinganisha na kuni za misituni, bidhaa hii ina uwezo wa kupunguza kwa gharama kwa asilimia 20,” anabainisha.

Swai anatoa mfano namna Kuni Poa zilivyotumika wakati wa wiki ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani nchini Tanzania.

Mjasiriamali huyo anasema kuwa idadi kubwa ya majiko yaliyotumika kuchomea nyama katika wiki hiyo, iliyoadhimishwa kitaifa jijini Arusha, yalikuwa yakitumia Kuni Poa.

Mwanzo mgumu

Hata hivyo, kama anavyobainisha mwenyewe, haikuwa kazi rahisi kwa watu kuanza kuielewa na kufumbata kuni hizo, kwani uelewa wa matumizi yake ulikuwa bado uko chini.

“Tulianza kutembelea taasisi mbalimbali za elimu tukitoa mafunzo kwa wapishi wa taasisi kuhusu matumizi ya Kuni Poa,” Swai anasema.

Hadi kufikia sasa, kampuni ya Hanny G, imefanikisha kutoa mafunzo ya matumizi ya nishati hiyo kwa wapishi zaidi ya 60 nchi nzima, huku kampuni hiyo ikizifikia asilimia 90 ya taasisi za elimu zinazoendeshwa na serikali.

Kupitia mafunzo yaliyotolewa na kampuni hiyo, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kilifanikiwa kujenga majiko banifu 102.

 Kukua kwa biashara

 Kwa sasa, kampuni ya Hanny G inashirikiana na shule za sekondari zaidi ya 475 nchini Tanzania, magereza 17, vyuo vya elimu 25 na vyuo vikuu viwili.

Swai anafikiria kuikuza biashara, hata ikibidi, siku moja ivuke mipaka ya Tanzania.

“Ajenda ya nishati safi ya kupikia ndio gumzo la mji kwa sasa, nadhani hali ni hiyo hiyo kwa nchi jirani pia,” anasema Swai, ambapo kupitia kampuni yake, ameweza kutoa ajira za kudumu 90.

Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ajenda mahususi ambayo imechukua nafasi kubwa katika Sera, Mipango na Mikakati ya Serikali mbalimbali duniani kwa sasa.

Umuhimu wa suala hilo unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi.

Kwa upande wake, lengo namba 7 la Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa limejikita katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati nafuu, inayopatikana kwa urahisi, endelevu na ya kisasa kwa wote.

Hata hivyo, bado kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa nishati nafuu, endelevu na za uhakika kwa ajili ya matumizi mbalimbali hususan ya kupikia hasa kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania.

Ni kwa hitajio hilo, serikali ya Tanzania , iliandaa  Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao unatoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi­ ya kupikia.

Mkakati huu una lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati sa­ ya kupikia i­kapo mwaka 2034.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us