Katika hali ya kuonyesha upendo na mshikamano, mashirika ya misaada ya Uturuki yamekuwa yakitoa misaada kwa wale wenye mahitaji barani Afrika katika kipindi cha sherehe za Eid al-Adha.
Shirika la Dini la Kituruki (Turkiye Diyanet Vakfi) na mashirika mengine ya misaada ya Uturuki, yamechinja zaidi ya mifugo 9,000 na kugawa nyama kwa familia zisizojiweza nchini Uganda ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sikukuu ya Eid al-Adha.
Mratibu wa masuala ya dini wa Uturuki nchini Uganda, Ramazan Pehlivanoglu, ameiambia TRT Afrika kwamba, zaidi ya ng’ombe 7,500 walichinjwa na nyama yake kusambazwa na shirika la Diyanet katika maeneo mbalimbali ya nchi. Ameongeza kuwa walionufaika zaidi ni wale wasiojiweza.
Kwa upande wao, mashirika ya misaada ya Tebessum na Iraji yamechinja ng’ombe 600, na kusambazwa nyama mashariki mwa Uganda.
“Tumechinja ng’ombe 600; lengo letu ni kufikia wasiojiweza, ikiwemo wakimbizi, wayatima, na familia zisizojiweza,” Uthman Muki, mkurugenzi wa Shirika la Iraji ameiambia TRT Afrika.
Ukarimu wa hali ya juu
Ameongeza kuwa, mbali na usambazaji wa nyama, pia walipewa vifurushi ya Eid, vilivyokuwa na mchele, mafuta ya kupikia, sukari, pamoja na nguo.
Abubakar Byango, mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Maendeleo la Byango, ameiambia TRT Afrika kwamba, kwa msaada wa Shirika la Uturuki la Keskul walichinja ng’ombe 350, mbali na kondoo 850, na kusambaza nyama kwa wenye mahitaji mashariki mwa Uganda.
Wengi wa waliopokea, wameelezea shukrani zao kwa ukarimu wa jumuia ya Uturuki.
Jitihada kama hizo pia zimefanywa katika nchi nyengine za Afrika kama vile Somalia, Tanzania, Kenya na Nigeria.
Hili linafanyika wakati ambao ushirikiano kati ya Uturuki na mataifa ya Kiafrika unaendelea kukua katika nyanja tofauti, ikiwemo shughuli za kibinadamu.
Balozi wa Uturuki nchini Uganda, Fatih Ak, amesema mbali na chakula, hatua hiyo pia inatoa ujumbe wa ukarimu na mshikamano ambao unavuka mipaka.
“Sisi, watu wa Uturuki, tunaojulikana kwa ukaribu wetu, tunafuraha kupeana hasa wakati wa sherehe za Eid al-Adha na Eid al-Fitr,” Balozi Ak ameiambia TRT Afrika.
Amesema hatua hiyo, inatokana na misingi ya dini ya Kiislamu na inaashiria misingi ya ulimwengu ya kuoneana huruma.
Athari ya kiuchumi
“Huu sio mchango tu, ni ishara ya udugu,” amesema Balozi Ak.
“Kinachofanya mchango huu kuwa na athari zaidi ni kwamba michago inatoka kwa wafugaji wa Uganda wenyewe. Hii inawainua wafugaji wa ndani, na kuwasaidia kukuza biashara zao,” amesema.