Afrika
3 dk kusoma
Afrika yaadhimisha siku ya Wangari Maathai, mtetezi wa mazingira
Mnamo Januari 2012, Umoja wa Afrika (AU) uliidhinisha 3 Machi kuwa Siku ya Mazingira ya Afrika na pia Siku ya Wangari Maathai kwa kutambua mchango mkubwa wa marehemu Profesa Wangari Maathai wa kutetea mazingira.
Afrika yaadhimisha siku ya Wangari Maathai, mtetezi wa mazingira
Wangari maathari arudi nyumbani baada ya kushinda tuzo la Nobel Disemba 2004
3 Machi 2025

Afrika inaadhimisha siku ya Wangari Maathai , Mkenya aliyetambulika duniani kwa kupaza sauti kutetea mazingira.

“ Leo, tunaheshimu maisha na urithi wa Profesa Wangari Maathai, kiongozi mwenye maono, mwanamazingira, na mwanamke wa kwanza Mwafrika kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel. Kujitolea kwake kusikoyumba kwa uhifadhi wa mazingira, maendeleo endelevu, na haki ya kijamii kunaendelea kutia moyo vizazi,” Tume ya Umoja wa Afrika umesema.

Kazi ya Wangari Maathai

Profesa Wangari Maathai, alianzisha shirika lililoitwa Green Belt Movement, Shirika lisilo la Kiserikali la mazingira lililojikita katika kushughulikia kupinga ukataji miti na uharibifu wa mazingira .

“ Wangari Maathai aliona kwamba dunia itakuwa jangwa. Aliwataka wanawake kutoka vikundi vya wanawake aliyokuwamo kuanza kupanda miti,” Cyrus Kimamo, katibu wa bodi ya Green belt Movement amesema.

Maathai aliangazia athari kubwa ya uharibifu wa mazingira hasa katika maisha ya wanawake wa vijijini ambao walibeba mzigo mkubwa wa athari mbaya ya mazingira kwa kilimo na upatikanaji wa chakula na hivyo kusababisha kunyimwa haki.

“ Mwanamke wa kwanza Mwafrika kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel, Wangari Maathai alijitolea kwa maendeleo endelevu na kukuza sauti za vijana ili kukuza amani,” Shirika la Nobel limesema.

Profesa Wangari aliongoza mapambano ya kulinda maeneo ya vyanzo vya maji yanayotetea upandaji miti, uhifadhi wa mazingira, na haki za wanawake nchini Kenya.

"Inakuja wakati ambapo ubinadamu unatakiwa kuangazia kiwango kipya cha fahamu ... wakati huo ni sasa." - Prof. Wangari Maathai aliwahi kusema.

Alihamasisha Wakenya, hasa wanawake, kupanda zaidi ya miti milioni 30, na kuhamasisha Umoja wa Mataifa kuzindua kampeni ambayo imechangia upandaji wa miti bilioni 11 kote ulimwenguni.

Kazi zake nyumbani

Zaidi ya wanawake 900,000 wa Kenya inaripotiwa walinufaika na kampeni yake ya upandaji miti kwa kuuza miche kwa ajili ya upanzi upya.

Umoja wa Mataifa unasema Maathai alitambua kwamba uongozi wa kisiasa wenye kusudi unaweza kufikia mabadiliko chanya ya kijamii.

"Kwa hivyo, mti ukawa ishara ya mapambano ya kidemokrasia nchini Kenya," Maathai alisema.

Aliandaa maandamano dhidi ya Rais wa zamani wa Kenya Daniel arap Moi, ambaye alimtaja kwa hasira kama "mwanamke mwendawazimu" na shughuli zake kama "uasi."

Mnamo 1992, wakati akipinga ugawaji wa ardhi wa rais kwa wasaidizi wake, alipigwa na majambazi na polisi wa serikali hadi akapoteza fahamu. Lakini alibaki imara .

Kutambuliwa kimataifa

Mnamo 2004, alikuwa mwanamke wa kwanza wa Kiafrika kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mchango wake katika "maendeleo endelevu, demokrasia na amani".

Aliandika vitabu kadhaa vikiwemo: The Green Belt Movement; Unbowed: A Memoir; The Challenge for Africa; and Replenishing the Earth.

Maathai aliaga dunia Septemba 2011 akiwa na miaka 71.

Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us