Video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii inaonesha baadhi ya watalii waliokwenda kuangalia msafara wa nyumbu katika hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya, wakiwatatiza wanyama hao waliokuwa wakivuka Mto Mara kutokea Tanzania.
Kanuni za uhifadhi, zinakataza watalii kushuka katika magari yao wawapo hifadhini, lakini hawa walionekana kukiuka agizo hilo hivyo kuwafanya baadhi ya nyumbu hao kushindwa kuvuka.
Tayari Wizara ya Utalii na Idara ya Wanyama Pori (KWS) pamoja na Serikali ya Kaunti ya Narok wametoa maagizo kwa makampuni ya utalii na wahusika wote kuhakikisha usalama wa wanyamapori pamoja na watalii kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Tukio hilo limeibua hasira mitandaoni kutoka kwa mashirika ya kuhifadhi wanyamapori.
Mwezi Julai , tukio kama hilo lilitokea nchini Tanzania ambapo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) liliwaonya wanaotoa huduma za watalii kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa ikiwemo kutoruhusu watalii kutoka nje ya magari yao pindi wanapoangalia uhamiaji wa kihistoria wa nyumbu kutoka Serengeti nchini Tanzania hadi Masaai Mara Kenya.