Wawakilishi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda wameafikiana kuhusu makubaliano ya amani yanayolenga kumaliza mapigano mashariki mwa DRC - yanayotarajiwa kutiwa saini 27 Juni, taarifa ya pamoja ilisema.
Makubaliano hayo, ni muendelezo wa maazimio yaliyotiwa saini mwezi Aprili, "yanajumuisha kuheshimu mipaka na kusitishwa kwa uhasama" huko mashariki mwa DRC, kulingana na taarifa iliyotolewa na mataifa hayo mawili, pamoja na Marekani na Qatar, waliokuwa wapatanishi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio atakuwepo kwenye hafla ya kutia saini makubaliano hayo baadaye mwezi huu jijini Washington, taarifa hiyo ilisema.
Kujumuisha waasi
Maelezo hayo yanajumuisha "kuachana, kusalimisha silaha, na kujiunga na vikosi vya taifa bila masharti kwa wapiganaji wenye silaha."
Kundi lenye silaha la M23 - ambalo wataalamu wa Marekani na Umoja wa Mataifa wanasema wanapata mafunzo ya kijeshi kutoka Rwanda - lilifanya mashambulizi mwanzo wa mwaka huu mashariki mwa DRC.
Lilichukua udhibiti wa mji wa Goma kufikia mwisho wa mwezi Januari kisha wakachukua mji wa Bukavu, na kuweka mifumo ya utawala katika maeneo hayo.Maelfu ya watu wameuawa.
Mashariki mwa DRC ambako kuna utajiri mkubwa wa raslimali, ni karibu na mpaka wa Rwanda, na kumekuwa na machafuko kwa miongo mitatu.
Kuhusika kwa Rwanda
Rwanda imesema mwezi uliopita kuwa makubaliano ya amani ya kumaliza migogoro na jirani zake yatatiwa saini katikati mwa mwezi Juni jijini Washington.
Rwanda inakanusha kuwasaidia kijeshi M23 lakini inasema kwa muda mrefu usalama wake umekuwa ukitishiwa na makundi yenye silaha mashariki mwa DRC, hasa kundi la FDLR, kundi ambalo lilianzishwa na watu wa kabila la Wahutu waliowaua Watutsi wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda 1994.