Kitambulisho cha kwanza cha taifa cha kidijitali cha Rwanda kinatarajiwa kupitia awamu ya majaribio ya usajili kabla ya kuanza kutolewa, kwa takriban mwezi mmoja. Hii ni kulingana na afisa wa Wakala wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wamesema.
Kwa lengo la kurahisisha ufikiaji wa huduma za umma na miamala ya kidijitali, kitambulisho kipya kitapatikana katika miundo mbalimbali: kadi halisi iliyopachikwa msimbo wa QR, toleo la mtandaoni, pamoja na nambari ambayo inaweza kutumika kuthibitisha utambulisho wa mtu mtandaoni.
"Tutafanya majaribio katika baadhi ya tovuti chache nchini. Tutakuwa na maafisa kwenye vituo, wanaozunguka kufanya uandikishaji huu wa awali. Lakini wakati huo huo, wale ambao wanataka kufanya uandikishaji wa awali bila kupitia mawakala wetu, wanaweza kufanya hivyo wenyewe," Josephine Mukesha, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA alibainisha.
Amefafanua kuwa awamu ya awali ya uandikishaji unalenga kuwaruhusu wananchi kuhakiki taarifa zao za utambulisho ambazo tayari ziko kwenye sajili ya NIDA.
Mchakato huo unajumuisha kuthibitisha majina, majina ya wazazi, mahali pa kuzaliwa, hali ya ndoa, anwani na taarifa nyingine muhimu.
Kitambulisho hicho, maafisa wanasema, kitasaidia shughuli na huduma za mtandaoni kwa kuwezesha uthibitishaji wa mbali. Hii inamaanisha kuwa watumiaji hawatahitaji kuwepo na vitambulisho vyao ili kuthibitisha utambulisho wao wakati wa biashara ya mtandaoni.
Itajumuisha vipengele vya ziada vya kibayometriki, kama vile vipimo vya macho (kwa Kiengereza iris), na itatolewa kwa watu wa umri wote, ikiwa ni pamoja na watoto walio chini ya miaka mitano na hata watoto wachanga.
Hata hivyo, kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano, ni picha tu itahitajika.
Vitambulisho vya kwanza vinatarajiwa kutolewa mwaka ujao.