Gilbert Deya, muanzilishi wa kanisa la Gilbert Deya Ministries amefariki katika ajali mbaya katika barabara ya Kisumu kwenda Bondo Jumanne, polisi wanasema.
Bishop Deya, kama alivyo fahamika zaidi, anasemekana alihusika katika ajali ya magari matatu likiwemo gari lake aina ya Noah iliyoyumba na kugonga basi la chuo cha Moi pamoja na gari ya kaunti katika barabara kuu kutoka Kisumu kwenda Bondo.
Deya aliyejitangazia uaskofu, alipata umaarufu kutokana na ibada ya moja kwa moja kupitia televisheni.
Hata hivyo alitumbukia katika kashfa kubwa baada ya kulaumiwa kuhusika na biashara haramu ya watoto, ambapo anadaiwa aliwaiba watoto watano nchini Kenya na kuwauza Uingereza ambapo makao makuu ya kanisa lake lilikuwa.
Ukosefu wa ushahidi
Bishop Deya alirudishwa nchini Kenya kujibu mashtaka mwaka 2017 baada ya kushindwa kuzuia kurudishwa kwake kupitia mahakama.
Wanawake waliokuwa na matatizo ya kupata mimba ambao walihudhuria kanisa la Gilbert Deya Ministries huko Peckham, kusini-mashariki mwa London, waliambiwa wangeweza kupata watoto wa "miujiza".
Lakini watoto hao mara zote "walitolewa" katika kliniki za mtaani katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Upande wa mashtaka ulisema watoto hao waliibwa kutoka kwa familia maskini za Kenya.
Mnamo July 2023, mahakama ya Kenya iliyokuwa ikisikiliza kesi yake ilimuondolea mashtaka hayo kwa ukosefu wa ushahidi wa kutosha. Hata hivyo mkewe, Mary Deya, aliamua kukubali mashtaka na kupokea kutumikia kifungo cha miaka minne.