Takriban watu 60 wanahofiwa kutoweka baharini baada ya ajali mbili mbaya za meli katika pwani ya Libya katika siku za hivi karibuni, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji lilisema Jumanne.
IOM inasema kuwa moja ya ajali hizo za meli ilitokea Juni 12 karibu na bandari ya Alshab huko Tripolitania, shirika la Umoja wa Mataifa lilisema.
Ni watu watano pekee walionusurika waliopatikana na watu 21 waliripotiwa kutoweka. Miongoni mwa wanaohofiwa kufariki ni Waeritrea sita, wakiwemo wanawake watatu na watoto watatu, Wapakistani watano, Wamisri wanne na wanaume wawili wa Sudan. Utambulisho wa wengine wanne bado haujulikani.
Tukio la pili lilitokea Juni 13, takriban kilomita 35 (maili 22) magharibi mwa Tobruk ya Libya. Kulingana na manusura wa pekee, ambaye aliokolewa na wavuvi, watu 39 hawajulikani walipo.
Takriban watu 743 wamekufa kufikia sasa mwaka huu wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya, wakiwemo 538 kwenye njia ya Kati ya Mediterania, ambayo inasalia kuwa njia mbaya zaidi ya wahamiaji inayojulikana duniani.