Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko nchini Afrika Kusini, ambayo yameaharibu nyumba na kusomba basi lililokuwa na wanafunzi katika Mkoa wa Eastern Cape, imeongezeka hadi 49, waziri mkuu wa mkoa huo amewaambia waandishi wa habari siku ya Jumatano.
Oscar Mabuyane anasema miili ya wanafunzi wanne ilipatikana siku ya Jumatano, huku watatu wakiokolewa siku ya Jumanne na wengine wanne hawajapatikana bado.
Amesema watu 13 walikuwa ndani ya basi hilo, ikiwemo dereva na msaidizi wake.
Basi hilo lilikuwa likiwasafirisha wanafunzi katika shule moja mji wa Mthatha wakati liliposombwa na mafuriko wakati likivuka daraja Jumanne asubuhi.
Baadhi ya sehemu za Afrika Kusini kumekuwa na theluji, mvua, na upepo mkali tangu mwishoni mwa wiki, kusababisha mafuriko yaliyoharibu nyumba na miundombinu.
Mamia ya watu wamelazimika kuhama makazi yao katika mkoa wa Eastern Cape na sasa hivi wako katika kumbi za kijamii.
“Shughuli za uokoaji zinaendelea,” Mabuyane aliwaambia waandishi wa habari, walieleza mkasa huo kama moja ya janga hatari kuwahi kutokea kwenye mkoa huo.
Watu tisa wamethibitishwa kufariki siku ya Jumanne katika mkoa huo ambapo nyumba na magari yalikuwa yamezama kwenye maji kutokana na hali hiyo mbaya ya hewa.
Siku ya Jumatano Rais Cyril Ramaphosa alitoa salamu zake za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na wale walioathirika, kuwahakikishia raia kuwa serikali itawapa msaada.