AFRIKA
2 dk kusoma
ICC yawatia hatiani wawili kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa uhalifu wa kivita
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu imemhukumu afisa wa zamani wa soka kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na mwanamgambo kwa uhalifu wa kivita uliotekelezwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kati ya mwaka 2013 na 2014.
ICC yawatia hatiani wawili kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa uhalifu wa kivita
ICC ndiyo mahakama pekee huru duniani yenye uwezo wa kuwafungulia mashtaka watuhumiwa wa uhalifu mbaya zaidi duniani. / / Reuters
24 Julai 2025

Katika hukumu iliyosomwa Alhamisi, ICC ilimkuta na hatia Patrice-Edouard Ngaïssona, aliyewahi kuwa Waziri wa Michezo na kiongozi mwandamizi wa makundi ya wanamgambo, pamoja na Alfred Yekatom, mbunge wa zamani aliyekuwa akiyaongoza makundi hayo katika medani ya mapambano.

Yekatom alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa makosa 20 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, yakiwemo mauaji na mateso, huku Ngaïssona akihukumiwa kifungo cha miaka 12 kwa makosa 28 ya aina hiyo hiyo.

Wanachama wao walikuwa sehemu ya kundi la wanamgambo lijulikanalo kama anti-Balaka, yaani “wapinga mapanga,” lililojitokeza kama kundi la kujilinda dhidi ya waasi wa Seleka waliovamia mji mkuu Bangui na kumuondoa madarakani Rais wa zamani Francois Bozizé.

Mateso ya kutisha

Jaji mkuu wa kesi hiyo, Bertram Schmitt, alisoma maelezo ya kutisha ya ukatili uliotekelezwa na wanamgambo dhidi ya Waislamu waliodhaniwa kuwa wanachama wa Seleka.

Askari wa Yekatom walimtendea mtu mmoja kwa kumkata vidole vya mkono na miguu na sikio moja kabla ya kuwaua na kuwakata sehemu zao za mwili.

Yekatom alisikiliza hukumu hiyo bila hisia zozote, huku Ngaïssona akikubali kwa kuashiria kwa kichwa wakati adhabu yake ilisomwa.

Hata hivyo, Mahakama haikuwakuta na hatia ya baadhi ya makosa, Yekatom aliondolewa kosa la kuhusika na kuwatumia watoto kama askari, huku Ngaïssona akikwepa hukumu ya ubakaji.

Walikana mashtaka yote

Wawili hao walikana mashtaka yote yaliyowakabili. Yekatom alikabidhiwa kwa ICC mwishoni mwa mwaka 2018 baada ya kukamatwa nchini CAR kwa kosa la kufyatua risasi ndani ya Bunge.

Ngaïssona alikamatwa nchini Ufaransa mwezi Desemba 2018 na kukabidhiwa kwa ICC. Wakati huo alikuwa Rais wa Shirikisho la Soka la CAR na pia mjumbe wa bodi ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa ICC ilisema hukumu hiyo “inahakikisha haki za msingi za waathiriwa” na “inaangazia umuhimu wa kuwatofautisha raia na wapiganaji katika muktadha wa vita.”

'Kutambua madhila ya waathiriwa'

“Hukumu ya leo ni hatua muhimu ya kutambua madhara makubwa na mateso yaliyowakumba waathiriwa na jamii zilizoathiriwa katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati,” alisema Naibu Mwendesha Mashtaka, Mame Mandiaye Niang, katika taarifa yake.

“Adhabu hii ni ujumbe mzito kutoka kwa ICC kwamba wale wanaohusika na uhalifu wa kikatili unaotambuliwa chini ya Mkataba wa Roma watafikishwa mbele ya sheria na kuwajibika.”

Mahakama ya ICC ilianzishwa mwaka 2002 na ndiyo mahakama huru pekee duniani yenye mamlaka ya kuwafungulia mashtaka watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu mkubwa zaidi duniani.

InayohusianaTRT Global - Jamhuri ya Afrika ya Kati yamshikilia kiongozi wa waasi Sayo kwa uhalifu wa kivita
CHANZO:AFP
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us