Mkutano kati ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin, na mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, kabla ya mwisho wa mwezi Agosti, ni jambo lisilotarajiwa kufanyika, amesema msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov.
Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari mjini Moscow Ijumaa, Peskov alisema mkutano kati ya Urusi na Ukraine unapaswa kumaliza mzozo kwa kuweka masharti yote waliokubaliana rasmi.
“Je, mchakato huu mgumu sana unaweza kukamilika ndani ya siku 30? Bila shaka, hilo halitafanyika,” alisema Peskov alipoulizwa kuhusu uwezekano wa mkutano huo kufanyika kabla ya Agosti kuisha.
Wakati huo huo, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, Jumatano alisema kwamba Uturuki itajitahidi kuwaleta viongozi wa Ukraine na Urusi pamoja.
“Wiki hii, kupitia mazungumzo na Putin na Trump, tutaendelea kujitahidi kuona kama tunaweza kuwaleta viongozi hawa pamoja mjini Istanbul,” alisema Erdogan.
“Mawazo yanayokinzana”
Zaidi ya hayo, rasimu za mikataba kutoka Urusi na Ukraine zinakinzana kabisa, jambo ambalo linafanya isiwezekane kuoanisha mawazo yao kuhusu suluhisho kwa muda mfupi, Peskov aliongeza.
“Msimamto wetu unajulikana; umeelezwa katika rasimu ya makubaliano tuliyoitoa kwa upande wa Ukraine,” alisema Peskov, akiongeza kuwa pande zote bado zina kazi kubwa ya kufanya.
Urusi imedai kwamba Ukraine izingatie msimamo wa kutoegemea upande wowote na isiwe mwanachama wa muungano wowote wa kijeshi, pamoja na kusitisha uwepo wa majeshi ya kigeni katika ardhi yake.
Naye, Zelenskyy ameyataja masharti hayo kuwa ni kama shurutisho, na anataka kusitishwa kwa mapigano pamoja na mazungumzo ya ana kwa ana na Putin.
Tarehe 23 Julai, Istanbul ilishuhudia duru ya tatu ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Urusi na Ukraine kuhusu kutafuta suluhisho la mzozo.
Kabla ya kikao kikubwa, viongozi wa wajumbe, Vladimir Medinsky na Rustem Umerov, walifanya mazungumzo ya faraghani ya ana kwa ana.
Sehemu kuu ya mazungumzo ilidumu dakika takriban 40, ambapo pande hizo zilipitia na kuangalia nafasi zao kama zilivyoelezwa kwenye rasimu za makubaliano.