AFRIKA
5 DK KUSOMA
Mashairi bado yanaishi
Ikiwa dunia inaadhimisha siku yake ya Kimataifa, Machi 21, 'Ushairi', baadhi ya wataalamu wa Fasihi wanaamini kuwa bado tanzu hiyo ina nafasi yake katika jamii.
Mashairi bado yanaishi
Msanii Mrisho Mpoto kutoka Tanzania amejizoelea umaarufu kupitia ghani zake, ambazo ni sehemu za Fasihi simulizi./Picha: Anadolu Ajansi / Others
21 Machi 2024

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Miaka ya nyuma, iliyokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) , ambayo kwa sasa inajulikana kama TBC Radio, ilikuwa na kipindi maarufu cha 'Malenga Wetu'.

Kipindi hichi, cha takribani saa moja, kiliwaleta pamoja wataalamu wa mashairi kutoka Tanzania, wakichambua dhima za tungo mbali mbali na baadae kuzighani hewani kwa manufaa ya wasikilizaji.

Kikitiwa nakshi na Khalid Ponera na mwenzake Mohammed Ngombo, ambao pia, walikuwa ni wjauzi wa Ushairi, ama kwa hakika, kipindi hichi kilipata wafuatiliaji wengi sana, hasa ukizingatia kuwa kwa kipindi kile cha miaka ya 1980 kuelekea 1990, RTD ndio ilikuwa redio pekee kwa wakati huo.

Tanzu hii pia ilijizoelea umaarufu kwenye taasisi mbali mbali za elimu, kwani wanafunzi pia walifundishwa namna ya kutunga na kuandika mashairi, kwa kuzingatia vina na mizani, ambavyo vilikuwa ni vitu muhimu katika utunzi huo.

Washairi maarufu kama Sheikh Shaaban Robert, Profesa Mohamed Ilyas, Mohammed Seif Khatib na tungo kama Bahati haina Kwao, Titi la Mama Litamu na Chungu Tamu ni baadhi ya tanzu zilizopata umaarufu sana katika ukanda wa Afrika Mashariki, hasa kutokana na dhima zao na mchango wao katika kukuza lugha ya Kiswahili.

Mara kwa mara, yaliandaliwa matamasha makubwa ya Ushairi, yaliyowaleta pamoja manguli katika eneo hili, kwa lengo la kuburudisha na kuelemisha jamii.

Moja ya kumbi zilizoandaa matukio ya aina hii, ni ukumbi maarufu wa Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo wataalamu wa fasihi walikutana kusikiliza na kujadili dhima ya tanzu hii inayoakisi maisha ya binadamu.

Hata hivyo, pamoja na mabadiliko makubwa na ya kasi ya kiiteknolojia yanayoshuhudiwa ulimwenguni, baadhi ya wapenzi wa ushairi, bado wanaamini kuwa Tanzu hii ina nafasi yake katika maisha ya kila siku.

Nafasi ya Ushairi katika Jamii

Kulingana na Mgunga mwa Mnyenyelwa, msanii maarufu wa sanaa za majukwaani kutoka Tanzania, nyakati zote, kama ilivyokuwa huko nyuma, bado umuhimu wa ushairi uko palepale.

"Mashairi ya kijadi yalikuwa yanafuata mfumo wa vina na mizani, lakini tusisahau kuwa hata nyimbo za Bongo Fleva na nyinginezo bado ni ushairi unaofuata utaratibu wa tofauti, kwahiyo itoshe tu kusema kuwa Ushairi bado unaishi hadi leo hii," anaiambia TRT Afrika.

Mgunga, ambaye alipata umaarufu baada ya tungo yake ya Nenda Mwalimu, aliyoitoa baada ya kifo cha Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1999, anasisitiza kuwa Fasihi haipaswi kuwa kama maji kwenye mtungi, na hivyo ni vyema kubadilika kutokana na nyakati.

"Mashairi lazima yanyambulike, yaende kwenye kutongoa na kutamba, hatuwezi kuwa wafungwa wa jana kutokana na mabadiliko yanayoendelea sasa ulimwenguni," anasema.

Kulingana na Mgunga, Ushairi ni kama kazi ya Kimaabara ambayo inapaswa kuendana na kasi ya hadhira yake.

Wakati sehemu kubwa ya hadhira ikiwa imehamia kwenye mitandao ya kijamii, Mgunga anaamini kuwa wasanii wana kazi kubwa ya 'kupigania roho ya Ushairi', kuhakikisha kuwa inaendelea kukuza lugha na kuchokoza fikra.

Jitihada hafifu

Hata hivyo, pamoja na kuwa na majina maarufu katika nyanja ya Ushairi kama vile Profesa Mugyabuso Mulokozi, Kulikoyela Kahigi na Euphrase Kezilahabi ambao walikuwa ni manguli wa sanaa hiyo, Mgunga anaamini kuwa bado jitihada hazitoshi kuhakikisha kuwa Ushairi unaendelea kuishi.

"Wengi wanajitahidi kupokea vijti kutoka kwa manguli hao, lakini ukweli ni kwamba Ushairi bado una nafasi yake kwenye jamii," anaongeza.

"Natamani sana kufanya warsha kwenye taasisi za elimu."

Kwa upande wake, Ally Mirrow mfuatiliaji wa sanaa za majukwaani kutoka Tanzania anasema kuwa bado Ushairi una nafasi kubwa sana katika jamii.

Mirrow anatoa mifano ya vitabu vya ushairi vinavyotumika mashuleni kama sehemu ya uhalisia huo.

Kulingana na mpenzi huyo wa kazi za Kifasihi, tanzu hiyo bado inaendelea kukita mizizi katika sehemu za pwani ya Tanzania, kama vile katika maeneo ya Tanga na Zanzibar, wakati kwa upande wa bara, Mrisho Mpoto anaidhihirishia dunia umuhimu na nafasi kubwa ambayo ushairi inayo katika jamii.

Siku ya Ushairi Duniani

Siku hii ilipitishwa rasmi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mnamo mwaka 1999, katika kuunga mkono lugha tofauti kupitia ushairi na kuongeza fursa ya kuziokoa lugha zilizo hatarini.

Lengo la siku hii ni kuhamasisha usomaji, uandishi, uchapishaji na ufundishaji wa mashairi duniani.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us