AFRIKA
2 DK KUSOMA
Tanzania:CCM yataka kupuuzwa kwa kasoro ili kukuza demokrasia
Nchimbi amesema ni vyema TAMISEMI ikaangalia uwezekano wa kuwarudisha wagombea wote walioenguliwa kutokana na makosa hayo madogo madogo ili kuhamasisha ukuaji wa demokrasia kwenye uchaguzi huo.
Tanzania:CCM yataka kupuuzwa kwa kasoro ili kukuza demokrasia
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi nchini Tanzania, Dkt Emmanuel Nchimbi./Picha: @ccm_tanzania / Others
12 Novemba 2024

Chama tawala nchini Tanzania (CCM) kimeiomba Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuwaelekeza wasimamizi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kupuuza makosa madogo madogo yaliyotokea, ili kuruhusu wagombea wengi kushiriki uchaguzi huo.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Emmanuel John Nchimbi, ametoa mfano wa makosa ambayo yanapaswa kupuuzwa kuwa ni pamoja na wagombea kukosea herufi za majina.

“Waziri wa TAMISEMI tunajua anafuata sheria, lakini ni muhimu kutambua demokrasia yetu hii bado ni changa hivyo tunahitaji muda wa kuendelea kujiífunza…tunaziomba mamlaka hasa TAMISEMI katika nyakati za mwisho za rufaa kuyapuuza makosa madogo madogo ili watu wengi wapate nafasi ya kugombea", alisema Dkt Nchimbi, wakati akizungumza na wahariri wa habari jijini Dar es Salaam, siku ya Novemba 12.

Kwa mujibu wa Nchimbi, ni vyema kwa TAMISEMI kuangalia uwezekano wa kuwarudisha wagombea wote walioenguliwa kutokana na makosa hayo madogo madogo ili kuhamasisha ukuaji wa demokrasia kwenye uchaguzi huo.

Aidha, kuhusu sehemu kubwa ya malalamiko mengi ya kuenguliwa kuonekana ni ya wagombea wa vyama vya upinzani, Nchimbi ametumia fursa hiyo kuwatoa wasiwasi Watanzania kuwa, si kweli kwamba wagombea walioenguliwa ni wale wa vyama vya upinzani pekee, bali wapo pia wagombea wa CCM waliowekewa vipingamizi vya kugombea.

Mara ya mwisho kwa Tanzania kufanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ilikuwa ni Novemba 2019.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni hatua muhimu kwa Tanzania, wakati taifa hilo likijiandaa kufanya Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us