Viongozi wa Afrika, wataalamu wa uchumi, na mashirika yasiyokuwa ya serikali wamekusanyika mjini Lomé, Togo, kwa ajili ya kongamano muhimu kuhusu madeni.
Huku kukiwa na deni linaloongezeka, kiwango cha riba na mabadiliko ya kisiasa, mkutano huu unaoanza 12 hadi 14 Mei, 2025, unatoa fursa kwa bara la Afrika kubadilisha mtazamo— wakiwa na muongozo wao wenyewe.
Kujifunza kutokana na historia
Afrika imeshawahi kujikuta katika hali kama hii. Mwanzo mwa miaka 1980, mataifa ya Afrika yalikuwa na deni kubwa lililosababishwa na viwango vikubwa vya riba duniani kutokana na bei ya mafuta.
Nchi nyingi zilikopa kwa uangalifu ili wawekeze katika miundombinu na kuondokana na kutegemea wakoloni kiuchumi.
Na wakati kukiwa na tatizo, mataifa ya Afrika yanakosa msaada wowote.
Kupitia Umoja wa Muungano wa Afrika (OAU) na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika (UNECA), viongozi walikuwa na mikutano kujadili madeni 1984, 1985, na 1987.
Walitaka kuwepo kwa kongamano la kimataifa kuzungumzia madeni barani Afrika, wakitarajia kufanya majadiliano na mashirika yanayotoa mikopo duniani. Wito huo haukuzingatiwa.
Matatizo ya kawaida
Miongo minne baadaye, ni kama mambo yako vile vile. Mabadiliko katika masoko duniani— mizozo ya kibiashara, ugonjwa wa COVID-19, mabadiliko ya tabianchi — yanasabababisha viwango vya riba kupanda.
Mataifa mengi barani Afrika sasa hivi yanalipa riba zaidi ya 10% kwa dhamana za chini ya miaka 10. Kulipa riba kubwa kwa madeni kunafanya taifa kukosa fedha za kufanya maendeleo, hata kama mkopo wenyewe ulikuwa kwa ajili ya masuala muhimu, kama vile nishati au miundombinu ya usafiri.
Hili silo tu tatizo linalojirudia - ni la kimfumo. Maendeleo ya Afrika yanahitaji zaidi ya mapato wanayokusanya.
Kwa mfano, Zambia inahitaji dola bilioni 7 hadi 11 kwa mwaka kwa ajili ya miundombinu —sawa na 26–38% ya mapato ya ndani wanayokusanya. 70% ya raia wake milioni 20 wanafanya kazi katika sekta ya kilimo isiyoingiza fedha, kujaribu kuongeza wigo wa kutoza kodi ili “wajitegemee” ni sawa na kufanya nchi hiyo kuwa na ligi mbaya zaidi ya mpira duniani au kuachana na mchezo huo kabisa.
Zambia haiko peke yake. Mataifa mengi barani Afrika inahitaji kukopa ili kujiimarisha —lakini mikopo iliyo bora, yenye usawa, na ambayo wanaweza kumudu kuliko iliyopo kwa sasa.
Kuweka katika mantiki ni kuwa, deni la Afrika kwa sasa liko katika viwango vibaya, na ni 10% tu ya madeni ya mataifa yanayoendelea. Ni karibu na kiwango cha deni la nje la Sweden au Brazil. Deni la bara la Afrika ni “tatizo” kwa sababu mifumo yake ya fedha imesababisha hali kuwa hivyo.
Mkutano wa Lome ni hatua muhimu
Kongamano la Lomé lilihitajika kufanyika muda mrefu ili kubadilisha mtazamo. Viongozi wengi wa Afrika wanataka kuwepo na agenda za misingi ambazo zinazungumzia umuhimu wa madeni na changamoto zake.
Miongoni mwa mada zitakazozungumzia:
Deni kama mbinu ya kimkakati: Deni ni baya, au ni muhimu kama mbinu ya kimkatati? Ni mbinu gani ambazo ni muhimu kimkakati kwa madeni? Ni masharti gani na vigezo ambavyo mataifa ya Afrika yanahitaji kusisitiza ili kupunguza gharama za mitaji, ikiwemo hatari za mabadiliko ya tabianchi?
Kuweka sawa mchakato wa mifumo: Nini mtazamo wa Afrika kwa mchakato wa haki, wa haraka na ulio sahihi kwa anayeomba mkopo? Wakopeshaji gani wana masharti nafuu? Namna gani ya kuwa na mfumo ambao utafanya mataifa yapate masharti nafuu kwa wanaotoa mikopo?
Kukabiliana na upendeleo: Mashirika ya fedha duniani kama IMF, Benki ya Dunia yanatathmini vipi bara la Afrika na suala la madeni, na masharti gani ya upendeleo yanahitaji kuondolewa? Ni tathmini gani ambazo taasisi za fedha zinaweza kufanya kuhusu Afrika, madeni na mtazamo wa dunia kuhusu Afrika?
Kufanya mabadiliko kuhusu mashirika ya fedha: Afrika itawezaje kutumia nafasi yake katika bodi hizo na katika G20 kuleta mabadiliko, hata kama wadau wakubwa watakataa?
Kuimarisha taasisi za fedha za Afrika: Mataifa ya Afrika yanahitaji kufanya nini kulinda taasisi za fedha za Afrika na mifumo yake? Vipi bara la Afrika linaweza kufanya mchakato wa haraka wa kuwa na shirika la fedha la Afrika (AMF), Benki ya uwekezaji ya Afrika na Benki Kuu ya Afrika?
Kuwezesha sekta binafsi: Vipi deni linaloweza kuelekezwa katika kuimarisha fursa za sekta binafsi – kwa mfano sheria za manunuzi, au kanuni za ushirikiano wa Serikali na mashirika binafsi? Nini cha kufanya kwa Afrika?
Mpango unaoongozwa na Waafrika wenyewe
Kongamano lililoandaliwa na Tume ya Umoja wa Afrika na mwenyeji wake Rais Faure Gnassingbé wa Togo, lina wito wa Afrika kwanza. Siyo kuhusu kutaka wahurumiwe au kuokolewa, lakini kutaka mfumo ambao unaongozwa na Waafrika ambao wanaona madeni kama njia ya kujiimarisha, wala siyo mtego.
Ni kuhusu kuwasilisha agenda zenye tija, ubunifu unaoongozwa na Waafrika wenyewe –kwa mfano kuwa na kundi la wanaotoa mikopo - ambalo linaangalia madeni mahsusi kwa Afrika wala siyo matatizo ya dunia, lakini kama njia ya kuleta ufanisi ulimwenguni.
Yatakayojadiliwa katika mkutano wa Lome, lazima yawe na dira kwa mijadala mingine duniani, kutoka kwa kongamano la kimataifa la nne la fedha kwa ajili ya maendeleo (FfD4) lililofanyika nchini Uhispania hadi kwa mkutano wa G20 nchini Afrika Kusini. Ujumbe wa Afrika uko wazi: ni wakati wa kuwa na makubaliano mapya kuhusu madeni.
Na kama msemo wa Kiafrika unavyosema, “Hadi pale simba atakapojifunza kuandika, kila simulizi itakuwa ikimpongeza anayewinda.” Kwenye Kongamano la Lomé, sisi tulioko barani Afrika tutaandika, na kuepuka historia isijirudie.
Mwandishi Hannah Wanjie Ryder ni Afisa Mtendaji Mkuu wa ‘Development Reimagined’
Kanusho: Maoni ya mwandishi hayaakisi maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.