AFRIKA
1 dk kusoma
Bunge la Kenya lapitisha Mswada wa Fedha wa 2025
Bunge la Kitaifa limepitisha Mswada wa Fedha wa mwaka 2025, baada ya kujadili na kukataa baadhi ya mapendekezo yaliyokuwa yangeongeza mzigo kwa walipa kodi. Mswada huo sasa unasubiri kutiwa saini na Rais ili kuwa sheria.
Bunge la Kenya lapitisha Mswada wa Fedha wa 2025
Bunge la Kenya limepinga pendekezo la kuipa Mamlaka ya Kukusanya Ushuru uwezo wa kufikia taarifa za kifedha za Wakenya. /Picha: X@NAssemblyKE / Others
19 Juni 2025

Miongoni mwa mapendekezo tata yaliyotupiliwa mbali ni lile lililopendekeza kuipa Mamlaka ya Kukusanya Ushuru Kenya (KRA) uwezo wa kufikia taarifa za kibinafsi na za kifedha za walipa kodi.

Pendekezo hilo lilikosolewa vikali na wadau mbalimbali kwa kuonekana kuvunja haki za faragha za wananchi.

Kwa mujibu wa Hazina ya Kitaifa, Mswada huo unalenga kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 24, kiasi kilicho chini ya makadirio ya awali ya Shilingi bilioni 30.

Mapato hayo yanatarajiwa kuwa sehemu ya makadirio ya Shilingi trilioni 3.316 ya mapato ya kawaida kwa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2025/2026.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Mipango, Mheshimiwa Kimani Kuria, alisema mnamo Juni 17 kwamba mswada huo unaonyesha makadirio ya mapato ya chini zaidi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ya juhudi za kuongeza mapato ya serikali.

Alifichua kuwa serikali ilikuwa ikitaka kukusanya Sh344 bilioni kutoka kwa Mswada wa Fedha uliokataliwa, 2024, na baadaye kutabiri mapato ya Sh49 bilioni kutoka kwa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Ushuru, 2024.

Katika mwaka uliopita, mswada wa fedha pia ulikumbwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi, hasa vijana wa kizazi cha Gen Z, ambao waliandamana kupinga baadhi ya vipengele vya mswada huo vilivyotajwa kuwa kandamizi.

InayohusianaTRT Global - Mswada wa Fedha Kenya, kwa nini unapingwa?
CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us