Shinikizo la bara la Afrika la kutaka uanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeendelea siku ya Jumatano huku mkutano wa 13 wa kamati ya Mawaziri wa Umoja wa Afrika ukiendelea nchini Zambia.
Mkutano huo katika mji mkuu Lusaka unaangazia kuwepo kwa nafasi za Afrika (CAP), ambao unataka kuwepo nafasi mbili za kudumu na tano za kubadilishana kwa bara hilo katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema alisema uwakilishi mdogo wa bara hilo katika baraza unakwamisha uthabiti wa Umoja wa Afrika katika kutatua migogoro na kuwepo kwa amani.
"Hili ni kweli kutokana na kuendelea kwa mapigano barani Afrika na kubadilika kwa hali ya kisiasa na kiuchumi duniani. Nchi za Afrika zinahitaji kuwa kitu kimoja na kujadiliana na makundi mingine kwa maslahi yao, hasa mataifa matano wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama," Hichilema alisema katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Ambrose Lufuma.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia Mulambo Haimbe anasema Afrika ndiyo bara pekee ambalo halina mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama, "jambo baya kihistoria ambalo limesababisha kuwepo kwa msukumo wa kutaka kufanyike mabadiliko ya baraza hilo."
Rais wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Philemon Yang anasema Afrika imetakiwa kuwasilisha mapendekezo yake ya kupigia debe uanachama wa kudumu kwenye baraza hilo.
"Ni mfumo ambao utasaidia Afrika kutetea nafasi yake ya kudumu kwenye baraza hilo, na kurekebisha ukosefu wa haki wa enzi za ukoloni na kutengwa," Yang alisema kwenye hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Ivor Fung, mkurugenzi katika ofisi yake.
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Mahamoud Ali Youssouf, akiwakilishwa na Kamishna wa Masuala ya Siasa, Amani, na Usalama(PAPS) Bankole Adeoye, amesema wito wa kutaka nafasi ya kudumu kwa bara hilo unakwenda sanjari na juhudi za kutaka kuhakikisha amani na usalama.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sierra Leone Alhaji Kabba, ambaye alikuwa mwenyekiti mwenza pamoja na Haimbe, aliunga mkono hoja hiyo.