Mamia ya watu wameuawa tangu mwezi Disemba katika migogoro iliyokithiri nchini Sudan Kusini kutokana na wizi wa ngombe na ulipaji kisasi, Umoja wa Mataifa ulisema Jumanne.
Mapigano kuhusu matumizi ya raslimali na wizi wa ngombe yamekuwa yakitokea sana katika nchi hiyo, ambayo pia yamesababisha ukame na mafuriko.
Mapigano miongoni mwa wafugaji yameongezeka Tonj Mashariki, katika Jimbo la Warrap kaskazini magharibi mwa Sudan Kusini, kusababisha "mamia ya vifo, uharibifu wa nyumba na watu wengi kuondolewa katika makazi yao," kulingana na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS).
"Mwezi Machi, watu zaidi ya 200 wanasemekana kuuawa wakati wa mapigano baina ya jamii tofauti," UNMISS ilisema kwenye taarifa.
Hali tete ya kisiasa
"Kunahitajika upatanisho wa haraka kwa serikali ya kitaifa ili kuepusha mapigano kufika katika viwango vibaya zaidi na kuleta jamii pamoja ili kumaliza matatizo yao kwa njia ya amani," alisema Guang Cong, naibu mwakilishi maalum wa UNMISS.
Mwezi Februari, afisa mmoja alikanusha kuhusu "uwagikaji damu mkubwa" katika jimbo la kusini Mashariki la Equatoria ambapo watu 41 ikiwemo wanawake na watoto waliuawa, huku wengine 65 wakijeruhiwa na wengine hawajulikani waliko, taarifa hiyo ilisema.
Mapigano hayo yamesababisha hali kuwa ya hatari zaidi Sudan Kusini, ambayo imekumbwa na hali tete ya kisiasa na machafuko ya kikabila tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Sudan 2011.
Taifa hilo pia limekuwa na mapigano kati ya vikosi vinavyomtii Rais Salva Kiir na hasimu wake wa muda mrefu, Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar.