Jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuwawekea shinikizo Tanzania ili iwachunguze maafisa wa polisi wanaodaiwa kuwanyanyasa kingono wanaharakati wa Kenya na Uganda mwezi uliopita, muungano wa mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya ulisema Jumanne.
Boniface Mwangi na Agather Atuhaire walizuiliwa katika mji wa kibiashara wa Tanzania, Dar es Salaam kati ya Mei 19 na 23 walipokuwa wanajiandaa kuhudhuria kesi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, ambaye anashtakiwa na uhaini na anakabiliwa na uwezekano wa hukumu ya kifo.
Wote wawili wameeleza kuhusu mateso na unyanyasaji wa kingono waliopitia mikononi mwa polisi waliowakamata.
Siku ya Jumanne, ‘Police Reforms Working Group’, muungano wa mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya, ulitoa wito kwa "Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jamii ya Kimataifa kushinikiza serikali ya Tanzania kuwawajibisha maafisa wa polisi na makamanda wao kwa mateso, dhulma, na unyanyasaji wa kingono dhidi ya Boniface Mwangi na Agather Atuhaire."
'Ukandamizaji wa kikatili dhidi ya' wakosoaji
Muungano huo pamoja na Chama cha Wanasheria nchini Kenya (LSK) katika mkutano na waandishi wa habari mjini Nairobi.
"Mateso na ukatili, unyama na udhalilishaji ni makosa makubwa ya jinai chini ya makubaliano na sheria kadhaa za kimataifa," walisema.
"Serikali ya Tanzania lazima iwakamate na kuwashtaki maafisa wote wa polisi wanaoshukiwa kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya Boniface Mwangi na Agather Atuhaire na kuwawajibisha kupitia haki ya mahakamani."
Irungu Houghton, mkurugenzi wa shirika la Amnesty International, Kenya, amesema Tanzania imekuwa ikifanya "ukandamizaji wa kikatili dhidi ya wote wale wanaowakosoa" ikielekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.
Rais Samia kushiriki uchaguzi
Rais Samia Suluhu Hassan anagombea katika uchaguzi lakini serikali yake imekipiga marufuku chama kikuu cha upinzani, Chadema, baada ya kudai mabadiliko kabla ya uchaguzi huo.
Serikali ya Tanzania haijajibu lolote kuhusu madai ya Mwangi na Atuhaire.