Serikali nchini Kenya imeagiza kuwa magari yote rasmi ya serikali yawe yamewekewa nambari za magari za kidijitali ifikapo tarehe 29 Agosti 2025.
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei aliagiza kuwekwa kwa nambari hizo zinazosemekana kuwa salama zaidi.
Alionya kuwa gari lolote la serikali ambalo halitotimiza masharti hayo kwa muda uliowekwa halitaruhusiwa kuwepo barabarani baada ya operesheni ya kitaifa inayoongozwa kwa pamoja na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) na Kitengo cha Kukagua Magari ya Serikali (GVCU).
Kila nambari ya kidijitali ina chipu iliyopachikwa na ina mawasiliano na setilaiti au mfumo unaoratibu, na kuruhusu ufuatiliaji wa kila hatua.
Teknolojia hii sio tu inasaidia katika kupata magari yaliyoibiwa lakini pia ufuatiliaji wa mienendo ya magari. Vibao vimeundwa kiasi kwamba ni vigumu kuchakachuliwa, na jaribio lolote la kuvibadilisha na kusababisha tahadhari kwa mamlaka.
Vibao vya awamu ya pili, vilivyozinduliwa mwaka wa 2023, vimeimarishwa zaidi na viko salama, ikiwa ni pamoja na mfumo wa ufuatiliaji kidijitali, na vimeundwa kukidhi viwango vya kimataifa vya utambuzi wa magari.
Kulingana na Koskei, muundo huo ulioimarishwa ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kukabiliana na uhalifu wa wizi wa magari, kuimarisha usalama barabarani, na kuhakikisha uwazi zaidi katika matumizi ya mali ya umma.
Uganda ilianza mfumo huo wa kidijitali Februari 2024 ikiangazia swala la usalama pia.