AFRIKA
4 dk kusoma
Kutimuliwa kwa Rasool Marekani kulipangwa na serikali ya Trump
Kwa kumfukuza Rasool, serikali imetuma ujumbe wa wazi: kuwa haitokubali mtu anayewakosoa, na kwamba wale wanaokataa kufuata msimamo wao watakabiliana na hatua kali dhidi yao.
Kutimuliwa kwa Rasool Marekani kulipangwa na serikali ya Trump
Marekani imemfukuza Balozi Ebrahim Rasool kwa madai ya kuieleza serikali ya Trump kama ya 'wazungu wabaguzi.' / TRT Afrika
24 Machi 2025

Na Ongama Mtimka

Licha ya kuwa taarifa rasmi inaonesha kuwa balozi wa Afrika Kusini nchini Marekani ametimuliwa kutokana na matamshi kuhusu serikali ya Marekani, kwa namna ambavyo uongozi huo ulivyojibu kuhusu kauli hiyo, kunaonesha kulikuwa na mpango wa kufanya hivyo na kwamba serikali hii imekuwa ikitaka mabalozi wajipendekeze kuliko kufuata diplomasia.

Kutimuliwa kwa Balozi Rasool siyo tu kujibu kilichotokea ila ni njama iliyoandaliwa kumuondowa mwanadiplomasia ambaye angekuwa mpatanishi muhimu kati ya Marekani na Afrika Kusini, ukizingatia msimamo wake wa kuheshimu sheria na uzoefu katika kazi yake.

Zaidi ya hayo, serikali ya Afrika Kusini haikuwa imefahamishwa kuhusu mipango ya kumtaka Balozi wao kuondoka.  Ilisikia kuhusu hilo kupitia mitandao ya kijamii wakati jambo lenyewe limeshafanyika.

Sera ya mambo ya nje ya uongozi wa Trump iko tofauti na majadiliano yaliyozoeleka ya kidiplomasia.

Badala ya kutatua tofauti zao na mataifa mengine, serikali hiyo inataka washirika wake pamoja na maadui zake kujipendekeza kwao.

Hatua hii inaonekana wazi na namna wanavyoshughulikia nchi ambazo hazitaki kuzingatia maslahi ya Marekani, hata wakati maslahi hayo yanagongana na maslahi ya mataifa yao au hayaendani na utaratibu wa kimataifa.

Kwa muktadha huu, kufukuzwa kwa Balozi Rasool kunaweza kuonekana kama njama pana ya kuwatenga wale wanaokosoa ubabe wa Marekani.

Pamoja na kuwa matamshi ya Balozi Rasool yalikuwa ya wazi na haki, hayakuwa chanzo kikuu cha kutimuliwa kwake.

Ila, yalichochea njama ambayo ilikuwa imepangwa na serikali ambayo ilikuwa tayari haimtaki Balozi, na kuamua kushughulika na makundi yasiyo rasmi badala ya kukubali juhudi zake za kutaka kukutana na uongozi wa serikali.

Matamshi yake yalidhihirisha wasiwasi kwa serikali ya Trump ambayo inaonesha dharau na kuishambulia Afrika Kusini mara kwa mara.

Kwa kumfukuza Rasool, uongozi huo umetuma ujumbe wa wazi: wakosoaji hawakubaliki, na kwa wale ambao wanakataa kufuata msimamo wao watakabiliwa na hatua kali.

Kutimuliwa kwa Balozi Rasool pia kunaonesha kuwa serikali ya Trump haiheshimu utaratibu wa kidiplomasia.

Kwa kuwa Afrika Kusini ilifahamu kuhusu hali hiyo kupitia mitandao ya kijamii, kuliko njia za kisawasawa za kidiplomasia, ni ishara kuwa serikali hii haizingatii itifaki wala kuwa na heshima.

Hatua hii inafanya Marekani ionekane kama isiyo mshirika mzuri kidiplomasia na pia imeonesha mfano mbaya wa namna inavyoshughulikia tofauti kati ya nchi mwenyeji na mwanadiplomasia.

Licha ya changamoto hizi, Afrika Kusini lazima ijibu kimkakati na kwa heshima ya kidiplomasia.

Kufukuzwa kwa Balozi Rasool kusijibiwe na hatua kama hiyo ambayo itaongeza hali ya wasiwasi na kuleta changamoto ya ushirikiano wa siku za baadaye. Badala yake, Afrika Kusini inatakiwa impeleke Balozi mwingine ambaye ataweza kukabiliana na mazingira magumu ya serikali iliyoko madarakani kwa sasa.

Mtu huyu lazima awe na ujuzi wa kucheza michezo ya kidiplomasia na uongozi ambao hautabiriki.

lengo liwe na kuwa na mkakati wa kufanikisha kuendelea kwa makini ili kulinda maslahi ya Afrika Kusini bila kukubali shinikizo la matakwa ya mataifa yenye uwezo duniani na kuachana na misimamo yake thabiti.

Jibu la Afrika Kusini pia lazima lioneshe dhamira yake ya kuheshimu utaratibu wa kimataifa pamoja na haki za binaadamu.

Nchi hiyo haiwezi kuwa upande wa nchi zenye uwezo kwa sababu tu zina uwezo. Ila, ni lazima iendelee kutetea haki na usawa, hata kama ikifanya hivyo inaiweka katika mazingira mabaya na Marekani na mataifa mengine yenye uwezo duniani.

Msimamo thabiti siyo tu unadhihirisha misingi ya Afrika Kusini lakini pia jibu sahihi kwa ubabe na udikteta unaooneshwa na ikulu ya Marekani.

Serikali hiyo inataka watu wajipendekeze badala ya kuzingatia diplomasia, kutoheshimu utaratibu wa kidiplomasia, na ubabe wake ni wazi kuwa sera ya mambo ya nje ya Marekani imebadilika chini ya utawala wa Rais Trump.

Afrika Kusini lazima ijibu tukio hili kwa kutumia mikakati stahiki, kumpeleka mwanadiplomasia atakayekabiliana na mazingira magumu ya serikali ya sasa ya Marekani na wakati huo huo kuhakikisha dhamira ya nchi ya kuheshimu usawa na haki za binadamu.

Kwa kufanya hivyo, Afrika Kusini inaweza kuendelea kukabiliana na shinikizo la kujipendekeza kwa mataifa yenye uwezo na kulinda misingi yake katika dunia ambayo imegawanyika sana.

Mwandishi, Dkt Ongama Mtimka, ni mchambuzi huru wa masuala ya kisiasa nchini Afrika Kusini.

Kanusho: Maoni ya mwandishi hayaakisi maoni, mitazamo na sera za uhaririri za TRT Afrika.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us