Baba wa mchuuzi wa barakoa aliyepigwa risasi na polisi akiwa karibu wakati wa maandamano jijini Nairobi siku ya Jumanne amelaani kisa hicho.
Boniface Kariuki alikuwa akiuza barakoa alipokabiliwa na maafisa wawili wa polisi, ambapo mmoja wao alirekodiwa akimpiga risasi.
Akizungumzia matukio yaliyopelekea mwanae kulazwa hospitalini, Jonah Kariuki alisema polisi wanapaswa kujitahidi kuwalinda wanaofanya kazi kwa bidii ili kujikimu wao na familia zao.
"Ningeomba hawa askari waliofanya haya maneno wakome kwa sababu wanapiga watu wasio na hatia wenye wanaojitafutia mapato. Wakiwacha kuwaumiza itakuwa vizuri," alisema.
Muuzaji wa vinyago jijini kwa sasa anafanyiwa upasuaji, huku chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kikiandaliwa kwa ajili ya huduma baada ya upasuaji.
Hospitali ya taifa ya Kenyatta, KNH inasema katika taarifa kuwa Kariuki alifikishwa hospitalini saa tisa na dadika kumi na sita mchana siku ya Jumatatu.
“Alipofika katika kitengo cha dharura na ajali, alikuwa na majeraha ya risasi kichwani iliyopelekea majeraha ya ubongo na damu nyingi kuvuja,” Hospitali ya KHN imesema katika taarifa.
Uchunguzi ulithibitisha risasi ilikuwa imekwama upande wa kushoto wa kichwa. Mgonjwa alipekewa katika upasuaji na risasi ikaondolewa.
“Hata akiwa katika hali mahututi, yuko hai na anaangaliwa kwa karibu wakati wote,” taarifa ya hospitali ya KNH imeongezea.
Hospitali hiyo imesema ilipokea watu 16 waliojeruhiwa kwa maandamano.
“Majeraha hayo ni pamoja na majeraha ya risasi hadi kuumizwa kwa nguvu. Wagonjwa saba wamelazwa kwa usimamizi zaidi, tisa walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka, wawili wamefanyiwa upasuaji na wengine nne wamepangwa kufanyiwa upasuaji leo”, hospitali imeongezea
Kupigwa risasi kwa Kariuki kumezua taharuki miongoni mwa viongozi na Wakenya kwa jumla kuhusu mienendo ya polisi.
Huduma ya Kitaifa ya Polisi, katika taarifa siku ya Jumanne, ililaani kisa hicho na kusema afisa aliyehusika katika ufyatuaji risasi amekamatwa tangu wakati huo.
NPS ilisema Inspekta Jenerali Douglas Kanja aliamuru kukamatwa mara moja na kufikishwa mahakamani kwa afisa aliyehusika.