Vatikani siku ya Jumapili ilimtangaza kuwa mwenye heri mfanyakazi wa forodha wa Congo ambaye aliuawa kwa kukataa rushwa, na kuwapa vijana katika sehemu yenye ufisadi uliokithiri mtindo mpya wa utakatifu: Mtu ambaye alikataa kuruhusu mchele ulioharibika kugawiwa kwa watu maskini.
Mkuu wa Ofisi ya Watakatifu wa Vatikani, Kardinali Marcello Semeraro, aliongoza sherehe za kutangazwa kuwa Mwenyeheri Floribèrt Bwana Chui Bin Kositi Jumapili kwenye moja ya kanisa la Kipapa huko Roma, Mtakatifu Paulo Nje ya Kuta za Vatican.
Tukio hilo lilivutia shangwe kutoka kwa umati wa mahujaji wa Congo na jamii kubwa ya Wakatoliki wa DRC waishio Roma, ambao watapata mapokezi maalum Jumatatu na Papa Leo XIV.
Waaminifu walivalia fulana na vesti zenye picha ya Kositi na kushangilia kwa vifijo mara tu sherehe ya kumtangaza mwenye heri ilipokamilika, huku wakipeperusha bendera za DRC.
Alikataa kuruhusu mchele mbovu kupitishwa mpakani
Kositi alitekwa nyara na kuuawa mwaka wa 2007 baada ya kukataa kuruhusu mchele ulioharibika kutoka Rwanda kusafirishwa hadi katika mji wa Goma, mashariki mwa Congo.
Kama afisa wa serikali ya Congo ya kudhibiti ubora wa forodha, kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 alijua hatari za kukataa hongo zinazotolewa kwa maafisa wa umma. Lakini pia alijua hatari za kuruhusu chakula kilichoharibika kusambazwa kwa watu waliokata tamaa zaidi.
"Siku hiyo, wale wakorofi walijikuta mbele ya kijana ambaye, kwa jina la Injili, alisema 'Hapana.' Alipinga," rafiki yake Aline Minani alisema. "Na Floribèrt, nadhani kwangu binafsi, ningesema kwa vijana wote, ni mfano wa kuigwa."
Papa Francis anamtambua Kositi kama shahidi
Papa Francis alimtambua Kositi kama shahidi wa imani mwishoni mwa mwaka jana, na kumweka kwenye njia ya kutangazwa mwenye heri na pengine kuwa mtakatifu wa kwanza wa Congo.
Hatua hiyo ililingana na uelewa mpana wa papa kuhusu mfia imani kama dhana ya haki ya kijamii, ikiruhusu wale wanaodhaniwa kuwa wameuawa kwa kufanya kazi ya Mungu na kufuata Injili kuzingatiwa kuwa watakatifu.
"Nchi yetu inakaribia kushikilia medali ya dhahabu ya ufisadi miongoni mwa mataifa ya dunia," Askofu wa Goma Willy Ngumbi aliwaambia waandishi wa habari wiki jana. "Hapa, rushwa imeenea sana. Kwa hivyo, kama tungeweza kujifunza kutoka kwa maisha ya kijana huyu kwamba lazima sote tupigane na ufisadi ... nadhani hilo lingekuwa muhimu sana."
Transparency International mwaka jana iliipa Congo moja ya alama duni zaidi katika ripoti yake ya mtazamo wa ufisadi, ikiiweka 163 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa utafiti na 20 katika kipimo cha 0-100 cha shirika hilo, 0 fisadi mkubwa na 100 safi sana.
Mwana heri ‘Furaha ya Goma’
Kutangazwa mwenye heri kumeleta furaha kwa Goma wakati wa uchungu. Mapigano makali kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuuteka mji huo kumezidisha hali ambayo tayari ilikuwa moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani.
Imefufua matumaini ya watu wengi katika nchi ya zaidi ya watu milioni 100 ambao maendeleo yao yamezimwa na ufisadi wa kudumu, ambao Francis alikashifu wakati wa ziara yake ya 2023 nchini.
Akizungumza katika uwanja wa michezo wa Kinshasa wakati huo, Francis alisema Kositi "angeweza kufumbia macho kwa urahisi; hakuna mtu ambaye angegundua, na huenda hata angepanda cheo kama matokeo.
Lakini kwa kuwa alikuwa Mkristo, alisali. Aliwafikiria wengine na akachagua kuwa mnyoofu, akisema la, kwa uchafu wa ufisadi."