AFRIKA
3 dk kusoma
Rais wa Kenya atoa wito wa subira huku kifo cha mwanablogu kikichunguzwa
Albert Ojwang mwenye umri wa miaka 31, ambaye pia anasemekana kuwa mwalimu, alizuiliwa na polisi kutokana na ujumbe wake katika mtandao wa X ambao ulidaiwa kumkosoa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat, na baadaye akaripotiwa kufa.
Rais wa Kenya atoa wito wa subira huku kifo cha mwanablogu kikichunguzwa
Albert Ojwang alikufa akiwa chini ya ulinzi wa polisi/ picha: Wengine / Public domain
11 Juni 2025

Rais wa Kenya William Ruto amesema amesikitishwa na kifo cha mwanablogu Albert Ojwang ambaye alikufa akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

“Kama wakenya wengi na hasa kama mzazi, nilipokea habari ya kifo cha Albert Ojwang akiwa chini ya ulinzi wa polisi na mshtuko na mshangao.,” amesema katika taarifa.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 31, ambaye pia anasemekana kuwa mwalimu, alizuiliwa na polisi kutokana na ujumbe wake katika mtandao wa X ambao ulidaiwa kumkosoa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat.

Baadaye alihamishwa zaidi ya kilomita 350 hadi mji mkuu, Nairobi, katika Kituo cha Polisi cha Central siku ya Jumamosi.

Polisi walisema baadaye alipatikana akiwa amepoteza fahamu kwenye seli yake akiwa na majeraha ya kujidhuru, kisha akaripotiwa amekufa.

Hata hivyo uchunguzi wa maiti ulionyesha Ojwang alikuwa na majeraha makubwa kichwani na sehemu zingine za mwili kuashiria kuwa alikuwa ameuawa.

Baadhi ya wananchi waliandamana 10 Juni 2025 baada ya matokeo ya uchunguzi wa maiti , wakidai polisi walimuuwa Ojwang.

Rais Ruto amekashifu mazingira ya kifo cha mwanablogu huyo mwenye umri wa miaka 31 akieleza kuwa ni jukumu la afisa wa polisi anapomkamata mtu yeyote kuhakikisha kuwa mtu huyo yuko salama anapokuwa chini ya ulinzi wake.

“Polisi ni mlinzi anayeaminika wa usalama wa watu na mali zote na lazima waimarishe jukumu hili kila wakati ili kuhakikisha na kudumisha uhalali na uaminifu machoni kwa watu,: Rais Ruto aliongeza.

Ameagiza polisi kushirikiana na Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) inayofanya uchunguzi ya kifo cha Ojwang.

“Jamii yenye uadilifu hujengwa juu ya msingi wa uwajibikaji na matumizi yasiyoyumba ya utawala wa sheria. Wacha tuhakikishe mchakato huu unafikia hitimisho lake vizuri,” Musalia Mudavadi , Waziri kiongozi wa Kenya amesema.

Uchunguzi wa wazi

Lawama ya kifo cha Ojwang imewekewa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat ambaye inadaiwa aliamuru Ojwang akamatwe, kwa madai kuwa alikuwa amechapisha habari za uwongo kumhusu.

Rais Ruto amesema anatarajia matokeo ya uchunguzi kuwa ya wazi na kweli.

Maafisa wa polisi waliokuwa zamu katika Kituo cha Central jijini Nairobi wakati mwalimu huyo Albert Omondi Ojwang alipopatikana amefariki wameitwa rasmi kwa ajili ya kutoa ufafanuzi zaidi.

Waliitwa na maafisa wa upelelezi wa Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendaji kazi wa Polisi (IPOA) ili kuhojiwa rasmi na kupata taarifa zaidi.

Timu hiyo inachunguza mauaji baada ya uchunguzi wa maiti kubaini kuwa Ojwang alinyongwa na kushambuliwa.

Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, DCI, Mohamed Amin walifika mbele ya bunge la Seneti la taifa kujibu maswali kuhusu kifo cha Ojwang.

“IGP Kanja, ni nani ambaye alichakachuwa picha za CCTV katika Kituo cha Polisi cha Central usiku ambao Albert aliuawa, na huwezi kutuambia kuwa hujui kwa sababu kutakuwa na tatizo,” Enoch Wambua, Seneta wa Kitui aliuliza.

“Bwana Amin, je, DCI anaweza kutoa picha za CCTV za Albert Ojwang alipokuwa akihamishwa kutoka Makao Makuu ya DCI hadi Kituo cha Polisi cha Central ili kubaini ikiwa alikuwa amekufa au yuko hai?” Okongo Omogeni, Seneta wa Kaunti ya Nyamira alimuuliza mkurugenzi wa DCI.

“IGP Kanja, taja majina ya maafisa wa polisi walioingia katika seli alimokuwa Albert Ojwang na kumuua,” Stewart Madzayo, Seneta wa kilifi alihoji.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us