Maji! Maji! Maji!
Walisikika wapiganaji wa jeshi la Kinjekitile Ngwale, wakati wa mapambano yao dhidi ya Wajerumani, yaliyotokea kati ya Julai 1905 na 1907.
Vita hivyo vilitokea ndani ya iliyokuwa ikifahamika kama Tanganyika, ambayo leo inajulikana kama Tanzania.
Nikurudishe nyuma kidogo. Baada ya kumalizika kwa mkutano wa kuigawanya na kuitawala Afrika, maarufu kama ‘Mkutano wa Berlin’, uliofanyika kati ya 1884 na 1885, mataifa makubwa ulimwenguni yalianza udhibiti wa nchi mbalimbali za Afrika.
Moja ya mataifa hayo ni Ujerumani, ambayo iliamua kutwaa nchi kadhaa zikiwemo Tanganyika, Rwanda, Burundi na sehemu ya Msumbiji.
Nchi nyingine ni Namibia, Cameroon na Togoland (muungano wa Ghana na Togo).
‘Sheria kandamizi’
Hata hivyo, udhibiti wa makoloni yao ukawa dhaifu, hasa kwa upande wa Tanganyika, na hivyo kuwalazimu kuanzisha sheria kandamizi.
Walianzisha ‘kodi ya kichwa’ mwaka 1898 huku wakitegemea nguvu kazi ya Watanganyika kwenye ujenzi wa miundombinu.
Ilipofika mwaka 1902, Gavana wa Afrika Mashariki Gustav Adolf von Götzen alivilazimisha vijiji vya wakati huo kulima pamba kama zao la biashara kwa ajili ya kuuzwa nje.
Kila kijiji kilipewa lengo la kulima pamba licha ya changamoto ya maji iliyokuwepo kwa wakati huo.
Mwanzo wa manung’uniko
Sheria hizo hazikupokelewa vizuri na wananchi wa maeneo hayo. Ilifikia kipindi wanaume waliondolewa kwenye kaya zao na kwenda kutumikishwa, huku wanawake wakichukua majukumu ya wanaume.
Ilipofika mwaka 1905, ukame mkubwa ukalikumba eneo la kusini mwa Tanzania, na ndipo mapambano dhidi ya Wajerumani yakaanza.
Mapambano
Akaibuka mtu mmoja, aitwaye Kinjekitile Ngwale, Mmatumbi aliyezaliwa katika kijiji cha Ngarambe, ambaye aliwaaminisha watu kuwa alikuwa na uwezo wa kuwadhibiti Wajerumani kwa ‘imani za kishirikina’.
Akijinadi kuwa alikuwa na mzimu wa nyoka aliyeitwa ‘Hongo’, Ngwale akajipa jina la Bokero na kujitapa kuwa yeye ndiye mteule atakayewashinda Wajerumani.
Ngwale, akajinasibu zaidi kuwa angeweza kubadilisha risasi za Wajerumani kuwa maji.
‘Mchanganyiko maalumu’
Alitengeneza mchanganyiko maalumu wa maji, mafuta na mtama, na kuwaambia wapiganaji kuwa risasi zisingewadhuru iwapo wangetumia, na ndipo kulipozuka vita vya Maji Maji.
Katika mapambano dhidi ya Wajerumani, wapiganaji wa Kinjekitile Ngwale, walitumia risasi na upinde, dhidi ya bunduki na mabomu ya Wajerumani.
Hata hivyo, watu wapatao 300,000 walipoteza maisha katika vita hivyo, ambavyo kwa kiasi kikubwa vilitawaliwa na njaa kali.
Kunyongwa hadi kufa
Mwezi Agosti 1905, mamlaka za Wajerumani zilimkamata Kinjekitile Ngwale na kumshitaki kwa uhaini.
Kabla ya kuuwawa kwake, Kinjekitile aliwaambia Wajerumani kuwa alikuwa amesambaza dawa hiyo katika eneo zima la kusini mwa Tanganyika.
Agosti 14, 1905, wapiganaji wa kabila la Wangindo, walishambulia msafara wa wamisionari na kuua watu wote watano, akiwemo aliyekuwa Askofu wa Kanisa Katoliki la Dar es Salaam, aliyejulikana kama Spiss.
Licha ya kifo chake, Kinjekitile Ngwale anafahamika kwa kuyaunganisha makabila ya eneo la kusini mwa Tanganyika na vile vile kuwa mtu wa kwanza kuleta utaifa ndani ya Tanganyika.
Vuguvugu la Majimaji pia lilileta mabadiliko katika sera za kisiasa na kiutawala ndani ya serikali ya kikoloni ya Ujerumani.
Jumuiya za kimataifa zilipigia kelele unyanyasaji wa Wajerumani dhidi ya jamii za Tanganyika, huku wakitaka sera za kikoloni za Wajerumani ziangaliwe upya.
Serikali hiyo ya kikoloni ‘ilijitahidi’ kufanya maboresho ya utawala wake, ikiwemo kusitisha ‘utumikishwaji wa kazi ngumu’.
Hata hivyo, mabadiliko hayakutekelezwa ipasavyo hadi baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia, ambapo Tanganyika ikawa chini ya Waingereza.