Kama unaishi pwani ya Kenya huenda ukawa umesikia kuhusu lahaja ya Kibajuni. Ni mojawapo ya lahaja za Kiswahili, lakini ina maneno na lafudhi yake ya kipekee.
Dunga ambaye ni mzaliwa wa Lamu, katika Pwani ya Kenya, kupitia mahojiano na TRT Afrika, ameeleza kujivunia kwake kutoka sehemu hiyo ya Kenya. Na vile vile kuukubali ubajuni.
‘’Najivunia kutumia lahaja yetu ya kibajuni, na kuiendeleza”.
Kando na kutumia lahaja ya kibajuni, Dunga amepata kujulikana na wengi kwa kuigiza kama mume mwenye wivu na mke wake.
“Ninamshukuru meneja wangu, Bwana Bujra Mohamed, ambaye amenishauri niigize kama mume mwenye wivu, kwa sababu ingeleta mvuto zaidi, hata hivyo uigizaji huo haukulenga tu kukuza lahaja ya kibajuni, bali kukuza maadili ya vile mume anafaa kumtunza mke wake”, Dunga ameieleza TRT Afrika.
Baahi ya kauli zake zilizopata umaarufu zaidi katika uigizaji wa Dunga ni kama ifuatayo:
“Unani nami bangabanga, uniendeme, dhalimu we, wataka kunifanya mimi duyuthi, mi si duyuthi ti, kila ndako uniendeme, bangabanga hunilichi. Wataka kunivundia ndoa yangu?”
Kwa lugha ya Kiswahili sanifu, anamaanisha, una nini na mimi wewe jini (mtu mbaya), wewe ni dhalimu, wataka kunifanya mimi mtu ambaye hana wivu na mke wake, mbona unanifuata kila mahali, wataka kunivunjia ndoa yangu?
Changamoto za kupotea kwa lahaja ya kibajuni
Sababu nyingine zilizochochea Dunga kuigiza kwa lahaja ya Kibajuni ni kutokana na hatari ya kuangamia kwa lahaja hiyo.
“Wabajuni ambao wako sehemu za Mombasa, watumia lahaja ya Kimvita kuliko Kibajuni, na hivyo lahaja ya Kibajuni imeanza kupotea.”
“Tofauti na watengeneza maudhui wengine Mombasa, nimetumia njia yangu maalum kuwapatia wafuasi wangu ladha tofauti”. Dunga anaeleza.
Sikudhania kama ningekuja na tamthilia ya namna hii, kwa kutumia lahaja ya kikwetu, watu watapenda zaidi,
Lahaja ya Kibajuni
Kibajuni ni lahaja ya Kiswahili inayozungumzwa na Wabajuni, jamii ya watu wa Pwani hasa kutoka Lamu, Kisiwa cha Pate, na hata sehemu za Kusini mwa Somalia kama Kismayo.
Lugha ya Kibajuni ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Wabajuni. Hata hivyo, lugha hii iko hatarini kupotea kwa sababu vijana wengi wanazungumza zaidi Kiswahili Sanifu au Kiingereza. Bila juhudi za kuhifadhi lugha hii, huenda ikapotea kabisa kwa vizazi vijavyo.
Wabajuni kama wanavyofahamika ni jamii iliyo na asili yake katika visiwa vya Bajuni, pwani ya Somalia, japo kutokana na uhamiaji wa miaka mingi wanapatikana katika pwani ya Kenya na baadhi nchini Tanzania.
Kutokana na asili yake ya Kibantu, lahaja ya Kibajuni imechukua maneno mengi kutoka lugha za Kiarabu na Kiafrika, ikionyesha mwingiliano wa kitamaduni na biashara kati ya Wabajuni na jamii za pwani.
Utajiri wa Kitamaduni
Mbali na lugha, Wabajuni pia wanajisifia utamaduni wenye historia ya muda mrefu.
Ustadi wa Wabajuni katika ufundi wa majahazi na usindikaji wa samaki umewaletea umaarufu, huku ngoma na nyimbo zao zikionyesha utajiri wa utamaduni wao katika sherehe za kitamaduni na matukio muhimu.