Waziri Mkuu wa Uganda, Robinah Nabbanja amefichua kuwa Baraza la Mawaziri linatarajiwa kujadili pengo la kifedha kufuatia kusitishwa kwa misaada ya nje na Serikali ya Marekani kwa ajili ya matibabu na kuzuia virusi vya UKIMWI nchini Uganda.
"Kusisitishwa kwa ufadhili wa USAID kumeathiri kwa kiasi kikubwa miradi ya kudhibiti UKIMWI Uganda. Ili kukabiliana na tatizo hili, zaidi ya dola milioni 130 (Shilingi bilioni 480) za ziada zinahitajika ili kuziba pengo la ufadhili na kuendeleza huduma muhimu,” Nabbanja ameliambia bunge.
Jibu lake lilifuatia swali kutoka kwa mbunge wa wafanyakazi Abdul Byakatonda.
"Je, ni hatua gani za haraka ambazo serikali inatekeleza ili kupunguza athari za kusitishwa kwa ufadhili na Marekani na kuhakikisha matibabu ya UKIMWI hayakatizwi kwa raia milioni 1.4?” aliuliza
Pia alitaka serikali kuelekeza mikakati ya kuwaokoa wale ambao sasa wamepoteza ajira baada ya shirka la USAID kusimasha sughuli zake.
“ Ni mikakati gani imewekwa kulinda kazi kwa watu au kujumuishwa tena kwa waliopoteza ajira zao, ili wapate ujuzi zaidi na kuwa miongoni mwa wahudumu wa afya ya jamii 12,551 wa Uganda, ambao kazi zao sasa ziko hatarini kutokana na kuondolewa kwa msaada huo wa Marekani?” aliuliza Byakatonda.
Mbunge wa wafanyakazi pia ametaka kujua iwapo “ serikali itazingatia kuanzisha Kikosi Kazi cha dharura cha kudhibiti UKIMWI kama ilivyokuwa kwa Uviko 19 ili kuhamasisha njia mbadala za ufadhili na kuendeleza huduma kwa wanaougua maradhi hayo.”
Waziri mkuu amesema serikali pia inashirikiana na wadau wa kimataifa na wa ndani ili kupata fedha za kuhakikisha kuwa miradi hiyo ya kudhibiti UKIMWI haikwami.
“ Wizara ya Afya inaandaa ripoti kwa ajili ya kulieleza baraza la mawaziri kuhusu suala hili na kupata mwongozo wa namna ya kutafuta fedha za kuziba pengo hilo la ufadhili,” Nabbanja ameongeza.