AFRIKA
5 dk kusoma
Nigeria yaadhimisha demokrasia huku Ikiwa na changamoto ya usalama
Pamoja na kuwepo kwa ishara ya Demokrasia kuna hali isiyoeleweka: Demokrasia ya Nigeria inatishiwa na kuwepo kwa hali tete ya usalama inayoendelea.
Nigeria yaadhimisha demokrasia huku Ikiwa na changamoto ya usalama
Tinubu akihutubia wanajeshi waliopelekwa jimbo la Katsina kufuatia mashambulizi ya wapiganaji kwa raia. / Bola Ahmed Tinubu/X
17 Juni 2025

12 Juni, 2025 Nigeria iliadhimisha miaka 26 ya utawala wa kidemokrasia ambao haujatatizwa— hatua kubwa inayoonesha uimara katika bara ambalo nchi nyingi zinakabiliwa na mapinduzi ya kijeshi na mifumo isiyokuwa thabiti.

Ikiwa nchi yenye demokrasia kubwa zaidi barani Afrika, muelekeo wa Nigeria ni muhimu—siyo tu kwa raia wake zaidi ya milioni 230, lakini pia kwa bara zima na jamii ya kimataifa.

Lakini pamoja na kuwepo kwa ishara ya Demokrasia kuna hali isiyoeleweka: Demokrasia ya Nigeria inatishiwa na kuwepo kwa hali tete ya usalama inayoendelea.

Kwa zaidi ya muongo mmoja, makundi ya watu wenye silaha yamefanya imani ya watu juu ya usalama kupungua na kudumisha ukuaji wa demokrasia pamoja na kutatiza juhudi za kimataifa kuunga mkono suala la utawala bora, maendeleo, na uthabiti katika kanda hiyo.

Hali hii inahitaji muamko mpya na mkakati mahsusi kutoka kwa washirika ulimwenguni.Hali ya Nigeria inatoa taswira ya usalama na demokrasia—na kucheleweshwa kwa mabadiliko.

Wakati Nigeria iliporudisha utawala wa raia 1999, dunia iliridhishwa kwa kile ilichoonekana kuondokana na kipindi cha miongo mitatu cha utawala wa kijeshi.

Tangu wakati huo, imefanikiwa kufanya uchaguzi mara sita na kubadilishana madaraka kwa njia ya amani..

Uamuzi wa 2018 wa kuhamisha siku ya Demokrasia kutoka 29 Mei hadi 12 Juni —kuadhimisha kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa 1993, ambao unatambulika kwa sehemu kubwa kama uchaguzi huru katika historia ya Nigeria — ilikuwa wazo zuri.

Iliwaenzi mamilioni ya raia waliokuwa na ari ya kuwepo kwa demokrasia waliokabiliana na utawala wa kidikteta na kútaka serikali ya utawala bora. Lakini ari hiyo haijaweza kugeuka na kuwepo kwa mabadiliko halisi.

Kwa raia wengi wa Nigeria, demokrasia haijafanikiwa kuwawezesha kupata suala la msingi: usalama.

Changamoto ya usalama kwa Nigeria ni kubwa sana.

Usalama ndiyo msingi thabiti wa demokrasia. Unatoa hakikisho la haki za uhuru ambazo ni taswira za jamii iliyo wazi na kutoa fursa kushiriki katika siasa na masuala ya kiuchumi.

Nchini Nigeria, kutokuwepo kwa usalama ni kikwazo cha uwiano katika uchaguzi, kujumuika kwa raia, na kupata haki.

Watu wanakuwa hawataki kupiga kura. Imani kwa taasisi za serikali, hasa polisi na mahakama, imepungua.

Serikali mbalimbali zimetambua tatizo hili na kulikabili kwa mikakati tofauti ya kiusalama, ikiwemo uwezo wa kijeshi.

Lakini njia inabaki kujibu mashambulizi na uwezo wote ukiwa kwa serikali kuu. Mfumo wa usalama wa Nigeria unaweka uwezo wote wa kijeshi kwa makao makuu Abuja—haina tija kwa jamii ambayo mfumo wake ni ugatuzi na wenye maeneo mengi kama Nigeria.

Changamoto za usalama za Nigeria zinakuwa na athari kote duniani. Kama sehemu ambayo ni muhimu kimkakati, uwezo wa Nigeria - au kushindwa kwake—kukabiliana na usalama kuna athari katika kanda nzima kwa watu, magenge ya ulanguzi, ugaidi wa nchi hadi nchi, na uthabiti wa vikosi vya kulinda amani. Washirika wa kimataifa pia ni wadau katika ustawi wa Nigeria.

Na ndiyo maana mabadiliko ya sekta ya usalama lazima yaondoke katika kutegemea sera za ufadhili hadi kwa jamii ya kimataifa kujadiliana na Nigeria. Muelekeo wa mabadiliko uko wazi:

●       Kuimarisha sheria: Kuweka sheria kutasaidia demokrasia katika sekta ya usalama ambayo itasaidia kuimarisha mifumo ya Demokrasia ya Nigeria.

●        Kuwa na sera ya polisi ya maeneo mbalimbali: Nigeria inatakiwa iwe na sera ya polisi katika maeneo ya majimboni ambapo watakuwa wanawajibika, watakuwa watu wa jamii hiyo, na kuwezeshwa kukabiliana na vitisho mahsusi.

●        Utawala wa sheria na uwajibikaji: Maafisa wa usalama lazima wafanye kazi zao kwa utaratibu unaofuatiliwa na raia, na wawajibishwe pale wanapokiuka sheria hizo. Maafisa wa usalama wanaofuata mfumo wa demokrasia hawawezi kufanya kazi zao bila utii wa sheria.

●        Mabadiliko katika sekta ya haki : Demokrasia ya kweli inahitaji kuwepo na mfumo sahihi; mahakama huru, kesi kufanywa kwa haraka, na raia waweze kupata haki.

●       Kulindwa kwa raia: Nchi salama lazima iwe nchi huru. Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, waandishi wa habari, na watetezi wa haki za binadamu lazima walindwe, siyo kunyanyaswa, wakiwa kama washirika wa kuhakikisha kuwepo kwa jamii salama.

●        Uhusiano wa mazingira na usalama: Uhusiano kati ya uharibifu wa mazingira na mapigano lazima utambuliwe na utatuliwe kupitia sera halisi na uthabiti wa uwekezaji.

●        Uratibu wa kikanda: Nigeria lazima ifanye kazi na mashirika ya kikanda kama ECOWAS, AES, Umoja wa Afrika, na mataifa yaliyoko kwenye Ziwa Chad kukabiliana na vitisho vinavyovuka mipaka kwa njia ya ushirikiano na kiintelijensia zaidi.

Jamii ya kimataifa—hasa mataifa washirika, taasisi mbalimbali, na mashirika ya fedha ya kimataifa—ina fursa ya kufanya mabadiliko. Hii inamaanisha kuwa na zaidi ya msaada wa muda mfupi na kuwa mipango ya misaada ya taasisi kwa muda mrefu. Ina maana kuainisha misaada na matokeo ya utawala bora.

Na inamaanisha kutoa kipaumbele kwa suala la usalama — usalama na heshima kwa watu.

Nigeria ina uwezo, watu, na ushawishi wa utamaduni kuongoza katika suala la demokrasia barani Afrika.

Ili kutimiza hilo, lazima itatue chanzo cha mzozo: kushindwa kwa nchi yenye demokrasia kuhakikisha usalama, haki, na fursa kwa wote.

Na huku Nigeria ikisubiri kuadhimisha miaka 27 ya utawala wa demokrasia, muda wa mabadiliko kwa ishara umekwisha. Kinachotakiwa kwa sasa ni utawala wa kuhakikisha usalama.

Kwa Nigeria, matokeo ya kutochukua hatua ni kumaanisha kuendelea kuwepo kwa hali tete, kuondoka kwa demokrasia, na kufifia kwa nafasi yake duniani.

Kwa jamii ya kimataifa, ni wazi: kuunga mkono demokrasia ya Nigeria kunamaanisha kuwaunga mkono watu wake waweze kuishi huru bila woga.

Usalama siyo mwisho wa demokrasia. Ni msingi hasa wa demokrasia. Na msingi huo lazima ujengwe —haraka na kwa ushirikiano

Mwandishi, Dkt. Kabiru Adamu, ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Beacon Security and Intelligence Limited, linalotoa huduma za utafiti wa masuala ya usalama na ushauri hasa katika maeneo ya Sahel.

 Kanusho: Maoni ya waandishi hayaakisi maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us