Wizara ya Afya nchini Uganda imetoa ufafanuzi kuhusu hali ya Uviko19 nchini humo. Katika taarifa yake imewahakikishia umma kwamba hakuna maambuziki mapya ya Uviko19.
“Hali ya kitaifa iko shwari na imedhibitiwa kikamilifu tangu mlipuko mkubwa miaka mitatu iliyopita,” Wizara hiyo imesema.
Taarifa hii imefuatia maelezo ambayo Wizara inadai yamewekwa katika mitandao tofauti ikiashiria kuwa kuna maambukizi mapya. Wizara imedai video hizo ni za zamani na potofu.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani- WHO, hadi mwisho wa 2023, Uganda ilikuwa na maambukizi 171,888 na vifo 3,632 kutoka kwa Uviko19.
Wizara hiyo imehakikishia umma kuwa hakuna maambukizi mapya ya ugonjwa huo ambao iliikumba nchi hiyo miaka mitatu iliyopita.
“Wizara inaendelea kuchunguza maelezo kuhusu aina mpya ya Uviko19 ambayo inaripotiwa katika sehemu tofauti duniani ikishirikiana kwa karibu na wadau muhimu ili kuhakikisha usalama wa umma,” Wizara hiyo imesema.
Uganda inasema ina mfumo dhabiti wa uangalizi ambao imeunda kwa muda mrefu dhidi ya magonjwa aina tofauti na ina uwezo muafaka wa kutambua maambukizi yoyote mapya kwa wakati.
“Mtu yeyote akiwa na ishara kama za homa inayohusishwa na Uviko19 ni vyema atembelee kituo cha afya kupata matibabu yanayofaa,” Wizara hiyo imesema.