MICHEZO
3 dk kusoma
Kenya, Tanzania na Uganda kuunda viza ya pamoja kwa ajili ya mashindano ya CHAN
Nchi hizo tatu zitaandaa mashindano ya kandanda ya kikanda mwezi Agosti 2025
Kenya, Tanzania na Uganda kuunda viza ya pamoja kwa ajili ya mashindano ya CHAN
Mawaziri wa michezo wa Kenya, Tanzania na Uganda wamesema nchi zao ziko tayari kwa mashindano ya CHAN Agosti 2025/ picha: Wizara ya michezo Kenya / Public domain
4 Juni 2025

Kenya, Uganda, na Tanzania zimesisitiza kuwa tayari kwa uwenyeji wa mashindano ya kikanda ya soka CHAN yatakayofanyika katika nchi hizi tatu.

Hii ni mara ya kwanza kwa nchi hizi tatu kuandaa mashindano haya pamoja.

“Huku zikiwa zimesalia chini ya siku 60, tumejitolea kukutana mara kwa mara ili kushughulikia masuala yanayoibuka kwa wakati halisi," Waziir wa Michezo nchini Kenya Mvurya alisema katika mkutano wa mawaziri wenzake kutoka nchi hizo tatu walipokutana jijini Nairobi.

Prof. Palamagamba Kabudi Waziri wa Michezo wa Tanzania na Peter Ogwang Waziri wa nchi wa Michezo Uganda walikuwepo.

Mawaziri hao wamekuwa wakikutana na ujumbe wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ukiongozwa na Katibu Mkuu Veron MosengoOmba, kujadili utayari wao kwa michuano hiyo ya kikanda ya Agosti 2025.

"Tumekubaliana kwa pamoja kutoa viza maalumu, PAMOJA VISA, ili kurahisisha usafiri katika mipaka yetu wakati wa mashindano. Maelezo yatawasilishwa hivi karibuni kupitia njia sahihi," Mvurya aliongeza.

Hii ni kwa ajili ya kuwezesha uratibu wa mpaka na kurahisisha wachezaji, viongozi na mashabiki kusafiri kwa urahisi wakati wa michuano.

Nchi hizo pia zimeafikiana kuhusu misamaha ya kodi na punguzo la kodi kwa uagizaji wa vifaa muhimu vinavyohitajika kwa shughuli za CHAN.

Zaidi ya hayo, nchi hizo tatu zitaanza majadiliano zaidi yaliyopangwa na shirikisho la soka la CAF wiki ijayo ili kukamilisha uidhinishaji wa kifedha wa bajeti ya pamoja unaokadiriwa kuwa dola milioni 39 na taratibu za matumizi yake.

Maafisa wa Kamati ya Maandalizi ya Ndani (LOC) kutoka nchi zote tatu wamepitia mafunzo ya usalama yanayoongozwa na CAF.

"Usalama unasalia kuwa kipaumbele kikuu. CAF imechukua mbinu madhubuti katika kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wetu wa LOC, kuhakikisha kuwa kila nchi inazingatia kanuni bora ili kuhakikisha mashindano salama," Mvurya alisisitiza.

Fursa ya kipekee kwa Afrika Mashariki

Waziri wa Nchi anayeshughulikia Michezo nchini Uganda, Peter Ogwang, alitoa mwaliko mzuri kwa mashabiki, timu, na washikadau kote barani na kwingineko.

"Tunatazamia kukaribisha kila mtu Afrika Mashariki kwa CHAN 2025. Haya si mashindano tu ni sherehe ya umoja wa Afrika, utamaduni, na vipaji," alisema.

“Kwa mashindano haya pamoja na yote yanasaidia nchi za Afrika Mashariki yamesidia sana nchi zetu kuja na miundombinu ya michezo na ya aina yake,” Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Michezo wa Tanzania amesema.

Ameongezea kuwa viwanja hivi katika nchi hizi tatu vinaweza kutumika tena baada ya mashindano ya CHAN na AFCON, kwa ajili ya michezo mengine baadaye.

“Ina maana kwamba CHAN ikiisha AFCON ikiisha bado tuna uwezo wa kufanya mashindano mengine mengi ya mipira au riadha,” ameongezea Kabudi.

“Michezo ni uchumi ni ajira lakini pia ni fahari, kwa hivyo sasa itakuwa ni fahari ya Afrika Mashariki,” Kabudi amesema.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us