Rais wa Chad, Mahamat Idriss Deby, Alhamisi alijibu hatua ya Marekani ya kuweka marufuku ya kusafiri kwa raia wa nchi yake kwa kusimamisha utoaji wa viza kwa raia wa Marekani.
"Nimeagiza serikali kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni za usawa na kusimamisha utoaji wa viza kwa raia wa Marekani," Deby alisema kupitia ukurasa wake wa X.
"Chad haina ndege za kutoa, wala mabilioni ya dola za kutoa, lakini Chad ina heshima na fahari yake."
Hatua hii ilikuja siku moja baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza marufuku ya kuingia Marekani kwa raia wa nchi 12, ikiwemo Chad, akisema hatua hiyo inalenga "kulinda" nchi yake dhidi ya "magaidi wa kigeni."
'Hatari kubwa'
Marufuku mpya ya kusafiri Marekani itaanza kutekelezwa kuanzia Juni 9.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani, tangazo hilo litazuia kabisa kuingia kwa raia wa nchi kadhaa, zikiwemo Afghanistan, Chad, Jamhuri ya Kongo, Guinea ya Ikweta, Eritrea, Haiti, Iran, Libya, Myanmar, Somalia, Sudan na Yemen.
Nchi hizi zimeonekana "kukosa vigezo vya uchunguzi na uhakiki" na zimeainishwa kuwa na "hatari kubwa sana" kwa Marekani, ilisema taarifa hiyo.