"Mwokozi amekuja. Amefungua macho ya watu. Amewaamsha simba waliolala. Sasa watanguruma, watanguruma kwa ushindi."
~ Ngũgĩ Wa Thiong'o katika kitabu chake cha ‘The River Between’.
Kwa wanafunzi wa Kiafrika katika miaka kati ya 1970-1990, maandishi kama haya yalikuwa kawaida kwao kutokana na kuwa vitabu vya Ngũgĩ Wa Thiong’o, vilikuwa vimesambaa na kufunzwa shuleni. Ngũgĩ, alikuwa miongoni mwa waandishi na wanachuoni maarufu walioibuka kipindi ambacho mataifa ya Afrika yalikuwa yanapata uhuru katika miaka ya 60 na 70.
Tabaka hili la wasomi lilijumuisha magwiji kama Chinua Achebe wa Nigeria na Profesa Ali Mazrui wa Kenya, walioibuka wakati Afrika ilikuwa ikijitafuta baada ya ukatili wa ukoloni na kuanza kurudisha lugha na utamaduni wake wa kabla ya utawala wa kikoloni.
Ngũgĩ wa Thiong'o, ambaye alifariki Mei 28 akiwa na umri wa miaka 87, alikuwa gwiji wa fasihi ya Kiafrika - msimulizi wa hadithi ambaye alifungwa jela, na baadaye kwenda kuishi uhamishoni.
Kazi yake ilichukua takriban miongo sita na tukiangalia maisha yake ni kama alikuwa anaandika kuhusu mabadiliko ya nchi yake - Kenya - pamoja na Afrika nzima, kutoka masuala ya ukoloni hadi demokrasia na mengine mengi.
Alizaliwa James Ngũgĩ mwaka wa 1938 katika eneo la Limuru, nchini Kenya. Alipokuwa mdogo alishuhudia udhalimu wa ukoloni katika nchi ya Kenya. Wazazi wake walijaribu kuweka akiba ya mapato yao madogo ili kulipia masomo yake katika Shule ya Upili ya Alliance, shule iliyoko karibu na eneo la Kikuyu.
Katika mahojiano, Ngũgĩ anakumbuka kurudi nyumbani kutoka Alliance mwishoni mwa muhula na kukuta kijiji chake kizima kimeharibiwa na mamlaka za kikoloni. Jamaa zake walikuwa miongoni mwa maelfu ya waliolazimika kuishi katika kambi wakati wa msako dhidi ya Mau Mau, vuguvugu la wapigania uhuru.
Katika mojawapo ya mateso makali zaidi, kakake Ngũgĩ, Gitogo, aliuawa kwa kupigwa risasi mgongoni kwa kukataa kutii amri ya askari wa Uingereza. Gitogo hakuwa amesikia amri hiyo kutokana na kuwa kiziwi.
Kutumia vitabu vyake vya kwanza, Ngũgĩ alitufunza kuhusu hali hii ya ukoloni kwa kuzungumzia jinsi jamii tofauti zilihangaika kukumbana na madhara yake. Katika ‘The River Between’, Ngũgĩ alionesha jinsi familia zilivyokuwa katika mvutano baina ya kufuata dini mpya iliyoletwa na wakoloni na kuendeleza mila na tamaduni za mababu zao.
Baada ya kumaliza shule ya sekondari, Ngũgĩ alipata ufadhili wa masomo katika Chuo Kikuu cha Makerere huko Kampala, Uganda 1959. Wakati wa kongamano la waandishi huko Makerere, Ngũgĩ alishiriki muswada wa riwaya yake ya kwanza na mwandishi anayeheshimika wa Nigeria Chinua Achebe. Achebe alipeleka muswada huo kwa mchapishaji wake nchini Uingereza na kitabu hicho, kwa jina ‘Weep Not, Child’, kikatolewa mwaka wa 1964. Ilikuwa ni riwaya ya kwanza ya lugha ya Kiingereza kuandikwa na mtu kutoka Afrika Mashariki.
Ngũgĩ aliandika riwaya zingine mbili maarufu zaidi, ‘A Grain of Wheat’ na ‘The River Between’. Mnamo 1972, gazeti la Times la Uingereza lilisema Ngũgĩ, wakati huo akiwa na umri wa miaka 33, "alikubaliwa kama mmoja wa waandishi bora wa Afrika".
Kuanzia 1964 hadi 1967, alisoma katika Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza, na kama akiwa Profesa kijana katika Chuo Kikuu cha Nairobi, aliandika "On the Abolition of the English Department," ilani iliyotetea fasihi ya Kiafrika kuwekwa katika mtaala wa chuo kikuu.
"Katika ushindi dhidi ya Wakoloni, lugha ilisaidia fikra kwa kile ambacho mapanga yalifanya kwa miili ya wakoloni." -Ngũgĩ Wa Thiong’o
Kisha 1977 - kipindi ambacho kiliashiria mabadiliko makubwa katika maisha na kazi ya Ngũgĩ. Kwa kuanzia, huu ndio mwaka ambao alikuja kuwa Ngũgĩ wa Thiong'o na kuachana na jina lake la kuzaliwa, James. Ngũgĩ alifanya mabadiliko kwa vile alitaka jina lisiloshabihiana na ukoloni. Pia aliacha Kiingereza kama lugha kuu ya fasihi yake na akaamua kuandika tu kwa lugha yake ya mama, Kikuyu. Alichapisha riwaya yake ya mwisho ya lugha ya Kiingereza, ‘Petals of Blood’, mnamo 1977.
Katika wakati huu, Ngũgĩ alitufunza kuhusu kuendeleza lugha na mila zetu kama Waafrika, akitumia kama njia ya mapinduzi dhidi ya ukoloni ya kifikra ambao ulikuwa umeanzisha lugha za kikoloni kuwa bora kuliko lugha zetu wenyewe. Kupitia hatua hii Ngũgĩ alikuwa akijikumbusha kuhusu utamaduni wake kupitia taaluma yake, akiwa anataka kuweka alama kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Mwandishi wa Kenya Carey Baraka alisema hivi kumhusu “kama lengo lake lilikuwa kuwafanya watu waandike kwa lugha ya mama, basi lilifaulu hata kama si kwa kiwango alichotarajia. Watu hao wote wanaoandika kwa lugha za asili kote ulimwenguni, wengi wao walihamasishwa naye.”
Hili lilidhihirika wakati Jalada, jukwaa la waandishi wa Kiafrika lilitafsiri hadithi yake fupi "Ituĩka Rĩa Mũrũngarũ," katika lugha zaidi ya 100. Munyao Kilolo aliyekuwa mhariri wa toleo hilo na alifanya kazi karibu na Ngũgĩ alisema, “hii ni hadithi fupi pekee iliyotafsiriwa zaidi katika historia ya uandishi wa Kiafrika. Na tafsiri nyingi zilikuwa katika lugha zingine za Kiafrika. Ulikuwa mradi maalum kwa sababu uliwezesha tafsiri kufanyika baina ya lugha za Kiafrika zenyewe, badala ya kupitia au kutoka kwa lugha za mataifa ya magharibi.”
"Walikuja usiku, wakiwa kimya, nyuso zao zikiwa zimefunikwa. Wale waliosema ukweli au kuhoji njia za mamlaka walitoweka na hawakuonekana tena. Kutokuwepo kwao kulikuwa onyo kwa wengine." Ngũgĩ Wa Thiong'o- ‘Petals of Blood’.
Vitabu vya awali vya Ngũgĩ vilikuwa vinakosoa serikali ya kikoloni, lakini kitabu chake "Petals of Blood" kilishambulia viongozi wapya wa Kenya iliyokuwa huru, na kuwaonesha kama tabaka la watu wa juu waliowasaliti Wakenya wa kawaida.
Ngũgĩ hakuishia hapo, mwaka huohuo, alishiriki tamthilia ya ‘Ngaahika Ndeenda (I Will Marry When I Want)’, iliyokuwa na taswira kali ya mapambano ya kitabaka ya Kenya.
Matumaini yake ya michezo ya kuigiza yalizimwa na serikali ya Rais wa wakati huo Jomo Kenyatta naye Ngũgĩ akafungwa jela mwaka wa 1977 bila kufunguliwa mashtaka sababu ikiwa tamthilia hiyo. Hata hivyo ilikuwa ni miezi 12 yenye matunda, - kwani Ngũgĩ aliandika riwaya yake ya kwanza ya Kikuyu, “The Devil on a Cross”, akiwa gerezani. Inasemekana alitumia karatasi ya chooni kuandika kitabu kizima, kwani hakuwa na daftari.
Hapa Ngũgĩ alitufundisha kuhusu kusimama kupigania haki hata dhidi ya wenye nguvu na kujitolea kwake kwa maisha ya Waafrika wenzake iwe kutoka kwa ukoloni au viongozi wapya baada ya uhuru.
“Kuna tofauti gani kati ya mwanasiasa anayesema Afrika haiwezi kuwa bila ubeberu na mwandishi anayesema Afrika haiwezi kufanya bila lugha za Ulaya?" Ngũgĩ aliuliza katika mkusanyiko wa insha, unaoitwa ‘Decolonising the Mind’.
Aliachiliwa kutoka gerezani mwaka wa 1978, na Ngũgĩ akaenda kuishi uhamishoni nchini Uingereza na kisha Marekani. Hakurejea Kenya hadi baada ya miaka 22.
Katika maisha yake yote - na hadi leo - fasihi ya Kiafrika ilitawaliwa na vitabu vilivyoandikwa kwa Kiingereza au Kifaransa, lugha rasmi katika nchi nyingi za bara. Katika wakati huo wote, na katika majukwaa na maandishi mbali mbali, Ngũgĩ alipigania vikali haki ya Waafrika kuenzi lugha zao badala ya lugha za kikoloni.
Katika hotuba iliyotolewa kupitia mkutano wa mtandaoni ulioandaliwa na Swahili Heritage Trust, Mombasa, tarehe 22 Juni, 2021, kusherehekea Siku ya Kiswahili.
“Ni kweli Kiingereza kinazungumzwa na watu wengi duniani kushinda Kiswahili. Lakini Kiingereza kilienea duniani kwa mabavu ya ukoloni na ubeberu. Si Kiingereza peke yake. Katika aina zote za ukoloni, au hali zote za watu fulani kuwakalia wengine, lugha hutumiwa kama fimbo ya kuzikandamiza akili za wanaonyanyaswa. Mkoloni huwafanya anaowatawala wazidharau lugha zao za mama na wazikumbatie kwa dhati lugha za kigeni za hao watawala wa kikoloni.”
Aliporudi Kenya, alikaribishwa kama shujaa - maelfu ya Wakenya walijitokeza kumpokea. Lakini kurudi kwake nyumbani kulikuwa na mkosi, alivamiwa na kushambuliwa pamoja na mke wake kubakwa.
Ngũgĩ alisisitiza kuwa shambulio hilo lilikuwa la "kisiasa". Alirudi Marekani, ambako alikuwa ni Profesa katika vyuo vikuu vikiwemo Yale, New York na California Irvine.
Baadaye katika maisha yake, afya ya Ngũgĩ ilidhoofika. Alifanyiwa upasuaji wacmoyo mara tatu mnamo 2019 akaanza kusumbuliwa na maradhi ya figo.
Mnamo 1995, aligunduliwa na saratani ya kibofu na kupewa miezi mitatu ya kuishi. Ngũgĩ alipona, hata hivyo, akiongeza saratani kwenye orodha ndefu ya mapambano ambayo alikuwa ameshinda.
Katika chapisho lake alilolitoa alipokwenda kumtembelea Ngũgĩ mwaka wa 2023, mwandishi Carey Baraka alieleza kuwa hakuwa anatoka sana nje ya nyumba, kutokana na maradhi yake.
"Siwezi kutoka nyumbani sasa kwa sababu ya ugonjwa wangu. Lazima uje kwangu. Mimi ndiye mfalme," alisema Ngũgĩ.
Kifo cha Ngũgĩ wa Thiong’o kilileta masikitiko makubwa kwa watu wengi na salamu za rambirambi zilitolewa na watu mbalimbali.
Munyao Kilolo alisema, “muhimu zaidi kwangu, alikuwa rafiki mpendwa na mshauri. Nitauheshimu urafiki huo na kazi tuliyofanya pamoja. Urithi wake utaendelea kupitia kazi kubwa aliyoiacha na yote aliyoyaacha.”
Winnie Byanyima, Mkurugenzi mtendaji wa zamani wa Oxfam na mke wa mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye alisema
“Gwiji wa Afrika na mataifa yanayoendelea, Ngũgĩ wa Thiong’o, amelala,- na kuondoka kwake, kumenifanya niwe mpweke ’’.
Tukiwa na umri wa miaka 13, tulisoma kitabu cha ‘The River Between’ darasani, na kwa miezi kadhaa tulikuwa matineja tuliokuwa na upendo wa Waiyaki na Nyambura. Kupitia hadithi zako za upole lakini zenye nguvu, ulifungua macho yetu kwa ulimwengu tuliokuwa tunautizama - kati ya mila na usasa, tamaduni zetu na Ukristo.
Zawadi kuu uliyonipa ni kitabu cha ‘Petals of Blood’, ambapo nilifahamu kwa mara ya kwanza kuhusu ukoloni mamboleo na usaliti wa wasomi wetu. Nilikufuata, nikasoma vitabu na insha zako… Ulinitengeneza mimi na kizazi changu.
Ngũgĩ wa Thiong’o, pumzika kwa amani. Pumzika kwa amani.”
Kifo chake kinatia ukomo wa maisha yaliyokuwa na zama tofauti, lakini jambo lililo dhahiri ni kwamba huu ndiyo mwisho wa maisha ya gwiji huyu aliyegusa maisha ya watu wengi wakati wa uhai wake na hata wakati huu ambapo amefariki.