Huku dunia ikiadhimisha siku ya wakimbizi 20 Juni, Afrika inabeba mzigo mkubwa wa wakimbizi.
Takwimu za umoja wa Mataifa zaonyesha kuwa kufikia mwishao wa 2024 takriban watu milioni 123 wamekimbia makazi yao barani Afrika.
Zaidi ya watu milioni 45.4 wamelazimka kuhama makazi yao barani Afrika, kati ya hao, milioni 12.2 ni wakimbizi huku wengine 32.2 wakiwa wakimbizi wa ndani.
"Kushindwa kwa diplomasia ya kimataifa na jitihada za kutatua migogoro na zaidi ya hayo kushindwa kuwalinda raia ni jambo la kushangaza,” amesema Jan Egeland, katibu mkuu wa shirika la Norwegian Refugee Council, NRC.
Wataalamu wanasema kuwa mzozo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imechangia pakubwa kwa idadi ya wakimbizi kuongezeka. Mwishoni mwa 2024, raia milioni 7.4 wa DRC walihamishwa kwa nguvu.
“Mgogoro wa muda mrefu kati ya jeshi la DRC na vikundi vingi vyenye silaha visivyo vya serikali umekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia unaendelea, na kusababisha moja ya migogoro mikubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani duniani,” Shirika la Kutetea Haki za Wakimbizi (UNHCR) limesema katika ripoti yake mpya ya hali ya wakimbizi duniani.
Mikoa ya mashariki ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yamekuwa kitovu cha ghasia nyingi katika miaka ya hivi karibuni.
Mnamo Februari 2024, kundi lenye silaha la M23 lilianzisha mashambulizi kwenye mji muhimu wa kimkakati wa Sake, na kuwalazimisha maelfu kukimbilia mji mkuu wa mkoa, Goma.
Kufikia mwishoni mwa 2024, Goma yenyewe ilikuwa imezingirwa na barabara nyingi za kuingilia mji huo zilikuwa zimefungwa, na kusababisha idadi ya watu ambao tayari wametengwa kunyimwa fursa ya ufikiaji wa bidhaa muhimu.
Ghasia zilizuka tena Januari 2025. Katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka, zaidi ya watu 660,000 walilazimika kukimbia maeneo ya pamoja ya muda huko Goma na viunga vya eneo la Nyiragongo.
Rwanda imelaumiwa na DRC kuwa inashirikiana na kikundi cha M23, hata hivyo Rwanda inaendela kukana madai hayo.
Nchi hizo mbili sasa ziko katika mchakato wa amani ambao unasimamiwa na Marekani.
Vita Sudan
Akiwa na miaka 75, Jermani Maria anasalia mkimbizi mwenye ujasiri na nguvu.
Jermani ambaye ni mkimbizi kutoka DRC, sasa amehamishwa tena hadi Sudan.
“Nilikuwa na hema kubwa katika makazi yangu huko Khartoum. Kabla ya vita nilikua napata samaki kutoka mtoni na kuuza,” Jermani anaelezea.
Sasa hivi anauza karanga ili kuweza kuwaangalia wajukuu zake.
Mnamo Aprili 2023, vita vya kikatili vilizuka nchini Sudan kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya RSF.
Miaka miwili baadaye, mzozo huo bado unaendelea kupamba moto. Imegeuza miji mikubwa kuwa viwanja vya vita, na vijiji na mashamba kuwa majivu.
Shule, hospitali, huduma za kuzlisha maji na umeme kadhaa zimeshambuliwa ikiwa ni pamoja na viwanda na masoko.
"Nilikuwa na ujauzito wa miezi miwili wakati watu wenye silaha waliingia kwetu, wakimtafuta mume wangu ili wamuue. Walikuwa wakiua wanaume wa kabila la Masalit, walitaka tu kutuangamiza. Lakini tuliwadanganya kwamba sisi ni wa kabila lingine, na tukafaulu kutoka hapo na kuvuka hadi Chad." Fatima, aliyelazimika kutoka Darfur amesema katika ripoti ya NRC.
Zaidi ya watu milioni 25 nchini Sudan sasa wanakabiliwa na njaa kali.
Shirika la NRC linasema kuwa takriban watu milioni tatu wametafuta hifadhi katika nchi jirani. Takriban milioni moja wamevuka kuelekea mashariki mwa Chad tangu kuanza kwa mzozo huo, huku maelfu zaidi wakiwasili kila wiki.
“Wengi wao ni wanawake na watoto, wamechoka kutokana na safari zao na sasa wanahitaji chakula, maji na ulinzi,” Ripoti ya NRC imesema.
Takriban robo tatu ya vituo vya afya havifanyi kazi tena. Magonjwa kama vile kipindupindu na surua yanaenea kwa kasi.
Katika mwaka uliopita, njaa imezidi kuongezeka katika maeneo kadhaa ya nchi, ikiwa ni pamoja na kambi ya Zamzam huko Darfur Kaskazini.
Uganda inahifadhi wakimbizi wengi barani Afrika
Uganda ndiyo nchi inayohifadhi wakimbizi wengi zaidi barani Afrika.
Sera zake za kimaendeleo zinazowapa wakimbizi uhuru wa kutembea, haki ya kufanya kazi, na kupata huduma mara nyingi huzingatiwa kama mfano wa kuigwa na ulimwengu.
“Lakini kiwango kikubwa cha wakimbizi na ufadhili duni wa muda mrefu sasa unaweka mkazo mkubwa kwa wakimbizi na jamii zinazowapokea,” NRC imeongezea.
2024 ilishuhudia kuzidi kwa wakimbizi wapya waliowasili kutoka Sudan, Sudan Kusini, DRC na kwingineko.
Idadi ya wakimbizi iliongezeka hadi milioni1.8, huku msaada wa chakula ukipunguzwa hadi dola 3 za Kimarekani kwa kila mtu kwa mwezi.
Huku idadi ya wakimbizi ikitarajiwa kuzidi milioni 2 ifikapo mwisho wa 2025 na ufadhili ukitarajiwa kupungua zaidi, hali inakaribia kudorora haraka.
Wataalam wanasema uamuzi wa Marekani kupunguza usaidizi wa kibinadamu unapunguza uwezo wa wakimbizi kupata mahitaji ya kutosha.
“Somalia na Sudan Kusini, ambako Marekani ilitoa viwango muhimu vya misaada, zimekuwa zikiathirika zaidi,” Ripoti ya NRC inasema.
Na hadhi ya Uganda kama mwenyeji mkubwa wa wakimbizi iko hatarini huku mashirika ya misaada yakipunguza misaada yao.