Afrika
6 dk kusoma
Uchumi endelevu msingi muhimu kwa Umoja wa Afrika kutafuta haki na usawa
Miundo ya kiuchumi inayoendeleza utegemezi wa misaada ya kifedha kwa Afrika ni aina moja ya udhalimu, ambayo inahitaji kuangaziwa kwa makini sawa na namna walivyojadili dhulma za kihistoria kwenye Mkutano wa AU Februari 2025.
Uchumi endelevu msingi muhimu kwa Umoja wa Afrika kutafuta haki na usawa
Utafutaji wa haki na usawa ndio msingi wa ajenda ya kisiasa ya Umoja wa Afrika (AU),
5 Machi 2025

Na Mubarak Aliyu

Umoja wa Afrika umeliwekea msisitizo suala la kutafuta haki na usawa, hasa kufuatia wito wa kutaka walipwe fidia kwa dhulma za kihistoria.

Hata hivyo, kufanikisha malengo haya makubwa kunategemea namna watakavyoshughulikia changamoto za kimuundo za kiuchumi ambazo zinaendelea kulemaza maendeleo ya bara hili.

Moja ya masuala yanayokabili nchi za Afrika ni changamoto za muundo wao wa upatikanaji wa fedha, kutokana na mikopo yenye riba kubwa, gharama kubwa za kulipa madeni, na masharti magumu ya mikopo.

Bila kushughulikia vizingiti hivi vya kifedha, dira ya AU ya kupata haki na usawa itakuwa ndoto tu ambayo haiwezi kutimia.

Mkutano wa hivi karibuni wa AU uliofanyika jijini Addis Ababa, chini ya kaulimbiu “Haki kwa Waafrika na Watu wa Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia,” ulionesha umuhimu wa kushughulikia dhulma za kihistoria.

Hata hivyo, mijadala kuhusu fidia lazima iambatane na kufanyia tathmini suala la kujitegemea kiuchumi na ukosefu wa usawa unaoendelea kuwa kikwazo kwa maendeleo ya Afrika.

Miundo ya kiuchumi inayoendeleza utegemezi wa misaada ya kifedha kwa Afrika ni aina moja ya udhalimu, ambayo inahitaji kuangaziwa kwa makini sawa na namna mkutano huo ulivyotaka suala la dhulma za kihistoria kutatuliwa.

Mzigo wa kiuchumi wa gharama kubwa za mikopo

Afrika ni bara ambalo linatumia sehemu kubwa ya fedha zake kulipa deni kiwango sawa na mapato wanayokusanya kwa jumla.

Kupungua kwa uwezo wa kifedha ni moja ya tatizo linalosababisha gharama za kukopa kuwa juu, huku serikali zikitenga sehemu kubwa ya mapato yao kwa kulipa madeni, na hivyo kubakisha fedha kidogo kwa ajili ya maendeleo.

Ripoti ya hivi karibuni ya Taasisi ya Mo Ibrahim ilionesha kuwa nchi 25 za Afrika zilitumia fedha nyingi zaidi za umma kulipa madeni ya nje kuliko kwenye suala la afya kati ya mwaka 2019 na 2021.

Matumizi haya ya rasilimali kwa masuala mengine, ni ishara ya namna sekta muhimu za kijamii zinavyopunjwa mgao, hasa sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii — ambazo ni muhimu katika kutatua suala la umaskini na ukosefu wa usawa.

Zaidi ya hayo, gharama kubwa za mikopo zinachangia kuwepo kwa deni kubwa.

Nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na viwango vya chini vya kuwawezesha kupata mkopo, jambo ambalo linasababisha riba ya juu wakati wa kuomba mkopo.

Hali inafanya nchi kuwa katika matatizo wakati wa kulipa deni na kulazimika kukopa tena.

Kulingana na Benki ya Dunia, zaidi ya nusu ya nchi zenye kipato cha chini barani Afrika kwa sasa ziko katika hali ya kushindwa kulipa madeni yao — huku kuyumba kwa uchumi wa dunia pamoja na misingi mibaya ya utawala bora ikichangia kwa hali hiyo.

Athari za kijamii na maendeleo kutokana na mzigo huu wa deni ni dhahiri. Kupeleka fedha nyingi katika kulipa madeni kunakwamisha uwekezaji katika sekta zinazokuwa, na hivyo kurudisha nyumba ukuaji wa uchumi.

Hii ni hatari hasa katika bara ambalo viwango vya umasikini bado ni vya juu na ambapo idadi kubwa ya watu wanategemea serikali kwa mahitaji yao ya msingi.

Masharti magumu ya misaada na demokrasia ‘isiyo ya hiari’

Taasisi za kifedha za kimataifa kama Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia mara nyingi hulazimisha mageuzi kama masharti ya kupata misaada kwa mataifa yanayoendelea ikiwemo Afrika.

Mageuzi haya kwa kawaida yanajumuisha hatua za kubana matumizi, maelekezo ya ubinafsishaji, na sera za kudhibiti soko kama masharti ya kupata msaada wa kifedha.

Sera za soko huria zimekosolewa sana kutokana na athari zake mbaya kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa viwango vya umasikini, kupunguza nafasi za ajira, na kushindwa kutoa huduma muhimu za umma.

Utafiti pia umehusisha ajenda ya kibepari na kurudisha nyuma kwa mafanikio ya kidemokrasia barani Afrika, kwani raia wengi wanahisi kutengwa na kutopata faida za demokrasia.

Mwanauchumi Thandika Mkandawire alielezea vyema hali hii kama “demokrasia isiyo ya hiari,” ambapo serikali za Afrika zinazotaka ufadhili zinalazimika kukubali maagizo ya viongozi wa taasisi za kifedha kutoka nje, na hivyo kuwaacha raia na mzigo wa deni.

Katika muktadha kama huu, mchakato wa kidemokrasia unakuwa hauna maana, kwani maamuzi muhimu ya kiuchumi yanafanywa na wataalamu kutoka nje na wala siyo serikali inayotakiwa kuwajibika kwa raia wake. Hili siyo tu inakwamisha uhalali wa kisiasa, bali unahatarisha usawa katika jamii.

Ili harakati za AU za kutafuta haki na usawa ziwe na maana, suala la kuwa na msingi endelevu wa fedha lazima lipatiwe umuhimu mkubwa.

Kutengwa kwa watu kwa misingi ya kiuchumi, ni aina moja ya kutokuwepo kwa haki na usawa masuala ambayo AU inataka kuyaondoa.

Mtazamo wa pande mbili katika kupata haki

Iwapo viongozi wa Afrika wanataka kufanikisha lengo la haki kupitia fidia, wanatakiwa kuwa na mtazamo wa pande mbili —moja inayoshughulikia dhulma za kihistoria huku ikikabiliana na dhulma za kiuchumi za sasa hivi.

Fidia kwa dhulma za kihistoria haitakuwa na mabadiliko ikiwa nchi za Afrika zitaendelea kuwa na madeni makubwa na kutegemea wengine kuimarisha uchumi wao.

Cha msingi kuwepo na haja ya kupatikana kwa fedha endelevu na kulipa kipaumbele suala la uhuru wa kiuchumi na kujiepusha kutegemea zaidi mataifa ya nje.

Mfumo huu lazima ujumuishe masharti mazuri ya mikopo, msamaha wa madeni, na upatikanaji wa fedha kwa masharti nafuu.

Nchi za Afrika pia zinatakiwa kuangalia mbinu za ubunifu za ufadhili, kama vile mifuko ya maendeleo ya kikanda na hati za dhamana za raia wake wanaoishi nje ya nchi, ili kuwa na vyanzo mbalimbali vya kuingiza mapato na kupunguza kutegemea mikopo kutoka nje.

Zaidi ya hayo, serikali za Afrika zinatakiwa kusisitiza katika suala la kuhakikisha linapata fedha za kutosha kwa kukusanya kodi za maendeleo, kuchukua hatua za kupambana na ufisadi, na urasimishaji wa uchumi usio rasmi.

Kuimarisha matumizi sahihi ya fedha za umma na uwazi katika michakato ya mikopo pia kutakuwa muhimu katika kuhakikisha kuwa fedha zilizokopwa zinatumika kwa malengo ya maendeleo badala ya kupotea kwa ufisadi au ubadhirifu.

Njia nyingine ya kuwa na fedha endelevu—moja ni inayoangazia msamaha wa deni, kujitegemea kiuchumi, na uwekezaji katika sekta ya kijamii—itatakiwa ili kuendeleza dira ya AU ya haki na usawa.

Bila kushughulikia vikwazo vya kifedha vinavyolemaza maendeleo ya bara hili, ahadi ya kupatikana kwa haki itabaki kuwa ndoto, na kutokuwepo kwa usawa itakuwa jambo la kawaida.

Kutaka kulipwa fidia lazima kuende sawa na uhuru wa kiuchumi—moja inayoweka mahitaji na matarajio ya raia wa Afrika katika ajenda ya maendeleo ya bara hili.

Mubarak Aliyu ni mchambuzi wa siasa na mwandishi wa masuala ya Afrika Magharibi na maeneo ya Sahel. Mada anazoziangazia ni pamoja na utawala bora na maendeleo kwa ujumla .

Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayaakisi maoni, mitazamo, na sera za uhariri za TRT Afrika.

Chanzo:TRT Afrika English

Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us