Viza za muda kwa raia wa Nigeria wanaotembelea nchini Marekani sasa zitakuwa hadi miezi mitatu tu, ubalozi wa Marekani katika mji mkuu Abuja, umetangaza.
Huu ni msururu wa hivi punde wa marufuku ya kusafiri na vikwazo vilivyotangazwa na Marekani, vingi kati ya hivyo vikiathiri nchi za Afrika.
"Kuanzia sasa, viza ambazo si za wahamiaji na si za wanadiplomasia zinazotolewa kwa raia wa Nigeria zitakuwa za kuingia nchini mara moja tu na muda wake hadi miezi mitatu," ubalozi wa Marekani nchini Nigeria uliandika katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne.
Hatua hii ilikuwa sehemu ya "orodha mpya ya (Marekani) kwa sera yake ya viza ya wasiokuwa wahamiaji, inayoathiri nchi kadhaa, ikiwemo Nigeria", iliongeza.
Marufuku ya kusafiri
Hapo awali, raia wa Nigeria waliotaka kusafiri hadi Marekani wangepata viza za muda mrefu kutokana na sababu za ziara zao.
Mwezi uliopita Rais Donald Trump aliwawekea marufuku ya kusafiri raia kutoka nchi 12, nyingi zikiwa kutoka Afrika, akitaja sababu kuwa ni za kiusalama na kutokuwepo kwa utaratibu sahihi wa kufanya ukaguzi.
Chini ya amri hiyo, raia wa nchi saba za Afrika - Chad, Jamhuri ya Congo, Guinea ya Ikweta, Eritrea, Libya, Somalia na Sudan -- walipigwa marufuku ya kuingia Marekani.
Kwa kulipiza, Chad ikasitisha mara moja kutoa viza kwa raia wa Marekani.
Serikali ya Nigeria haijajibu lolote kuhusu vikwazo vya hivi karibuni.
Lakini mwezi uliopita waziri wa mambo ya nje wa Nigeria alionya kuwa marufuku ya kusafiri na kuwekwa kwa kodi kutatatiza makubaliano ya kibiashara na nchi za Afrika Magharibi, hasa katika madini na nishati.