Mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yameweka rekodi ya namna vita vimeathiri mfumo wa elimu nchini Sudan.
Tangu kuzuka kwa vita mwezi Aprili 2023, takriban watoto milioni 19 hawako shuleni nchini Sudan.
Athari za vita zimekuwa mbaya kwa watu na miundombinu, huku 90% ya watoto wa umri wa kwenda shule wakiwa hawana fursa ya kupata elimu rasmi.
Madhara ya vita
Maendeleo duni ya mfumo wa elimu, miundombinu na kukosekana kwa vipaumbele vya programu za shule na ufundi, haswa kwa wasichana, kutaendelea kuathiri matarajio ya Sudan ya amani na utulivu.
Mnamo 2023, idadi ya watu wa Sudan ilikuwa milioni 43 na takriban 40% ya hawo ni chini ya umri wa miaka 15. Idadi ya watu nchini Sudan inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 75 ifikapo mwaka 2043 na 33% (takriban milioni 25) yawo ni chini ya umri wa miaka 15. Madhara haya yana athari mbaya kwa mustakabali wa Sudan.
Ongezeko la watu wenye umri wa kufanya kazi wanaokabiliwa na upungufu wa ufikiaji wa elimu bora huku kuzorota kwa viwango vya ubora wa elimu kunaweza kusababisha janga kubwa ikiwa hali hiyo haitodhibitiwa katika wakati muafaka.
Matokeo ya vita
Mfumo wa elimu wa Sudan umekuwa hatarini hata kabla ya kuanza kwa vita. Usumbufu na maandamano mengi yalisababisha kufungwa kwa shule na vyuo vikuu kwa miezi kadhaa.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya watoto milioni 3.6 (miaka 5-13) walikuwa nje ya shule kati ya 2020/2021. Ukosefu wa fedha na rasilimali za kutosha kuelekea miundombinu, ukuzaji wa mitaala na mishahara ya walimu pia zilikuwa changamoto zilizoathiri ubora wa mfumo wa elimu nchini.
Hii ni kwa sababu, kwa wastani, Sudan ilitumia 9% ya bajeti yake ya kitaifa katika elimu kwa kulinganisha na nchi nyingine za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo matumizi ya ndani ya elimu ni karibu 17%.
Katika kipindi cha sasa cha vita, pamoja na vifaa kuharibiwa kwa kiasi kikubwa, na watoto na walimu kuhamishwa, madhara yamekuwa makubwa huku shule nyingi nchini kote zikigeuzwa kuwa makazi.
Kuna mazingira machache salama ya kujifunzia, na hivyo kufanya iwe vigumu sana kwa mamlaka za mitaa na serikali kurejesha shughuli za elimu mijini na vijijini.
Ingawa mamlaka za kitaifa zimejaribu kutoa njia mbadala za shughuli za kielimu ikiwa ni pamoja na majaribio ya mtandaoni ili kuhakikisha kukamilika kwa mitihani, mbinu hizi hazizingatii tofauti kubwa za uwezo wa kifedha za jamii zaidi na hivyo kusababisha ugumu wa upatikanaji wa wanafunzi kwenye mtandao.
Kwa kuongezea, baada ya kutatizika kwa muunganisho wa intaneti na kuporomoka kabisa, huduma za satelaiti kama Starlink zimeibuka kama fursa na changamoto.
Makadirio ya siku zijazo
Njia ya kawaida ya kutathmini hisa ya elimu katika nchi ni kupima wastani wa miaka ya elimu kwa watu wazima (wenye umri wa miaka 15 na zaidi).
Data ya makadirio kutoka jukwaa la Taasisi ya Mafunzo ya Usalama ya African Futures zinaonyesha kuwa nchini Sudan, wastani wa miaka ya elimu kwa watu wazima inatarajiwa kuwa miaka 6. Hii inamaanisha kuwa watu wazima wengi watakuwa na elimu ya msingi ifikapo 2043.
Walakini, muundo huu wa utabiri ulitegemea data ya kiwango cha kitaifa iliyopatikana kabla ya kuanza kwa vita.
Takwimu za hivi karibuni na zilizopo kuhusu matokeo ya uhamiaji wa ndani nje ya nchi, uharibifu wa shule au matumizi ya shule kama makazi na rasilimali chache na uwezo duni wa wizara ya elimu ni masuala muhimu ambayo yanapaswa kushughulikiwa.
Hii inaweza kwanza kusaidia kutathmini kiwango cha uharibifu na kutoa maamuzi sahihi na suluhu kulingana na upangaji wa mustakabali.
Uwezekano ni kwamba watoto na vijana walio nyumbani, wenye uwezo mdogo wa kiuchumi, wanaweza kuajiriwa au kurudi katika vikundi vyenye silaha utaendelea kusababisha hali mbaya ya siku zijazo kwa amani, utulivu na ukuaji wa Sudan.
Kuandikishwa kwa watoto na vikosi vya jeshi na vikundi vyenye silaha ni jambo la kawaida na wasiwasi uliangaziwa mwanzoni mwa vita.
Mapendekezo
Katika muhula huu, mashirika ya kibinafsi na ya uhisani na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanapaswa kuzingatia ubunifu na uingiliaji kati wa haraka ili kutoa programu za elimu kwa watoto katika kambi za wakimbizi wa ndani nchini Sudan na wakimbizi katika nchi jirani ambapo wakimbizi wengi wamekusanyika.
Hii itaathiriwa na upunguzaji wa hivi majuzi wa misaada na fedha za maendeleo kote ulimwenguni, hata hivyo kuelekeza ufadhili wa kitaifa na kimataifa kuelekea kujenga upya mfumo wa elimu wa Sudan ni muhimu.
Jukumu pia lipo kwa Wizara ya Elimu ya Sudan kufanya kazi kwa ufanisi na kwa ushirikiano na washirika wa kimataifa ili kubuni mafunzo ya kimsingi kwa wanafunzi wa shule za msingi na mitaala ya ufundi kwa wanafunzi wa sekondari na vyuo vikuu.
Kuweka kipaumbele masuala haya ni njia pekee ya kuhakikisha elimu ya shule ya msingi kwa watu wazima wote ifikapo 2043.
Ujenzi mpya wa muda mrefu baada ya vita itabidi uzingatie na kuupa kipaumbele mfumo wa elimu.
Rasilimali za kutosha zinapaswa kutolewa ili kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa wote na kuimarisha ubora wa mitaala ya kitaifa kulingana na viwango vya kimataifa na mazoea bora na kubuni programu za elimu zinazohakikisha mabadiliko kutoka kwa mtoto, ujana hadi utu uzima kwa kuunda nguvu kazi yenye ujuzi na vifaa.
Kuwekeza katika elimu ni muhimu kwa ajili ya kujenga upya taifa la Sudan na kupata mustakabali wa watoto na vijana wake.