Mary Marwa alijifungua mtoto wake wa pili kwa dhiki. Ujauzito ulimsababishia tabu akiwa na wiki ishirini na nne tu na madaktari walishauri aitoe mimba hiyo baada ya kukutwa na ugonjwa wa ‘Help Syndrome’.
Lakini kama anavyosema, ilikuwa ni baraka kutoka kwa Mungu.
‘‘Madaktari walinishauri niitoe mimba na tukafanya hivyo. Lakini yule nesi aliyezoa vitu hivyo kwenda kutupa, aligundua mtoto yuko hai na akamhudumia mara moja na kumuweka katika mashine ya oksijeni, alimuokoa.’’ anasimulia Mary.
Japo habari ya mtoto kusalimika ingekuwa habari njema, ilikuja na changamoto baadaye.
‘‘Huyu mtoto amezaliwa miezi minne kabla ya wakati wake wa kuzaliwa na likizo yenyewe miezi mitatu. Na mimi bado singeweza kurudi kazini maana yule mtoto bado alikuwa mdogo sana siwezi kumuachia mtu. Ikabidi niwaombe pale kazini kama wanaweza kuniongezea miezi mitatu mingine bila malipo lakini walisema kwamba hawangeweza kwa sababu pia ni sheria. Ikabidi mimi niache kazi.’’ anasimulia Mary.
Lakini sasa afueni ya kisheria imepatikana. Kwa wazazi wanaojikuta katika hali kama ya Mary, wanafarijika kujua kuwa sheria ya kazi inawaruhusu kupewa muda wa ziada wa likizo kwa kujumuisha muda wa hadi mtoto atapotakiwa kuzaliwa kisha likizo baada ya hapo.
‘‘Kina mama wengi waliojifungua watoto kabla ya wakati wao, wataweza sasa kuwahudumia watoto wao kikamilifu kabla ya kurudi kazini,’’ anasema Dorris Mollel, mwanaharakati wa afya watoto njiti ambapo yeye mwenyewe alizaliwa kabla ya kukomaa.
Saini ya Rais
Sheria hii ambayo inasubiri tu saini ya Rais ili ianze kutekelezwa rasmi inaeleza kuwa likizo ya kujifungua itaanza kuhesabiwa baada ya mtoto kufikisha wakati wa kuzaliwa hata kama alizaliwa miezi kabla na itajumuisha wakati wote tangu mama kujifungua. Pia baba mtoto ameongezewa siku za likizo kutoka siku tatu hadi saba kwa ajili ya kumsaidia mama.
Kwa sasa kuna imani kuwa huu muda ulioongezwa utasaidia kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na ulemavu kwa sababu tu hawajapata muda wa kutosha kuangaliwa kwa namna changamoto yoyote ambayo ingejitokeza ingedhibitiwa mapema
‘‘Kwa mfano kuna mama namfahamu, aliporuhusiwa kwenda nyumbani mtoto wake alikuwa na kilo 1.8. Japo alishauriwa arejee hospitali kila baada ya wiki, hakuweza kwa sababu hakuwa na likizo kazini. Baada ya muda mtoto wake alipata ulemavu wa macho,’’ Doris anaambia TRT Afrika. ‘‘Lakini likizo hii itamuwezesha mama kumuangalia mtoto wake kwa makini mpaka akirudi kazini ameridhika,’’ anasema Doris.
Mfano wa kuigwa
Tanzania ni nchi ya pekee eneo la Afrika Mashariki kuweka sheria hiyo.
Lakini wanaharakati waliopigania marekebisho hayo, wanasema kuwa hawatakoma hapo, kwani kuna haja ya kuendeleza mjadala ili iweze kuigwa na mataifa mengine ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa manufaa ya kanda nzima.
‘‘Namna ambavyo Tanzania imeleta mfano kwenye marekebisho ya sheria ya uzazi, tunatamani pia Jumuiya ya Afrika Mashariki iweze kuiga mfano huo. Tunashirikiana na Bunge la Afrika Mashariki kuona namna hili linaweza kuwasilishwa kwa Jumuiya nzima,’’ Doris anaambia TRT Afrika.
Vifaa kusafishwa
Mbali na hilo, Doris anasema kuwa watasisitiza katika suala la ubunifu wa vifaa tiba katika vituo vya afya na zahanati.
‘‘Bado zahanati zetu hazina vifaa vya kuhudumia watoto wanaozaliwa njiti. Na sio hilo tu, hata watoa huduma hawana uelewa,’’ anasema Doris.
Tayari serikali ya Tanzania imetangaza kuwa kila hospitali ya Wilaya inatakiwa kuwa na vyumba maalum vyenye uwezo wa kuwaangalia kwa makini watoto njiti.