Na Abdalftah Hamed Ali
Bandari ya Sudan haikuwahi kuwa uwanja wa vita. Kwa miaka miwili, mji huo wa pwani ulikuwa umesimama kando na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea Sudan.
Mji huo ulikua kimbilio kwa wengi, kitovu cha utawala, na lango la mwisho la kufanya kazi kwa ulimwengu wa nje. Hayo yote yalisambaratika mnamo Mei.
Katika hali ya kushangaza, Vikosi vya RSF vilianzisha wimbi la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye jiji hilo mapema mwezi huu, na kugonga bandari yake, ghala za mafuta, na uwanja wa ndege pekee wa kimataifa.
Kwa raia wa Bandari ya Sudan, matokeo yamekuwa ya haraka na ya kikatili. Kukatika kwa umeme kumesababisha hospitali kuhangaika, familia bila friji au mawasiliano, na vitongoji vizima gizani.
Wafanyakazi wa misaada wanaripoti kuongezeka kwa hofu, huku huduma za kimsingi zikiporomoka na uhaba wa mafuta ukilemaza usafiri. Mashambulizi haya ya ndege zisizo na rubani yanakwamisha maisha ya raia.
Mashambulizi ya mapema mwezi huu yalisababisha vifo vya takriban raia 17, wakiwemo tisa waliokosa hewa kutokana na moshi wenye sumu.
Mashambulizi hayo yalizua hofu kubwa, huku zaidi ya kaya 550 kukimbia makazi yao, na kutatiza shughuli za kibinadamu.
Wakati huo huo, msaada wa kibinadamu lazima uimarishwe. Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada, ambayo tayari yamepanuliwa, yatahitaji mipango ya dharura kuweka misaada ili kusaidia Wasudan milioni 30 wanaohitaji - haswa katika mji wa Khartoum, Darfur, Kordofan, majimbo ya Kaskazini, na Al Gezira, na mamia ya maelfu wengine waliokimbia makazi yao Port Sudan na mazingira yake.
Kwa mara ya kwanza, ufuo wa mashariki wa Sudan umekuwa uwanja wa vita na RSF kwa makusudi kubomoa kile kinachoifanya serikali kufanya kazi: vituo vya nishati, vituo vya kusafiri, na njia za misaada ya kibinadamu.
Baada ya kupoteza ardhi huko Khartoum na mikoa ya kati, RSF sasa inapigana kutoka mbali.
Silaha yake mpya maalum ni ndege zisizo na rubani ambazo zinaweza kushambulia kwa umbali wa mamia ya kilomita, kudumaza mifumo ya nishati ya Sudan, minyororo ya usambazaji bidhaa, na njia za misaada ya kibinadamu bila kuwa na mwanajeshi hata mmoja ardhini.
Hesabu zao za kimkakati ziko wazi: epuka makabiliano ya moja kwa moja na vikosi vya juu vya jeshi, na badala yake kusambaratisha njia zainazo endesha harakati za mji .
Kampeni ya ndege zisizo na rubani ya RSF ni zaidi ya mabadiliko ya kimbinu, ni mkakati wa usumbufu wa mbali unaolenga kudhoofisha nchi baada ya kushindwa kuchukua udhibiti.
Kwa kutumia ndege hizo, RSF huepuka vita vya gharama kubwa huku ikisambaza hofu, kusitisha harakati za maisha na machafuko katika maeneo ambayo hayako chini ya udhibiti wao tena.
Miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa ni Kituo cha Wanamaji cha Flamingo, kituo kikuu cha jeshi la wanamaji la nchi hiyo kaskazini mwa bandari, kinacholengwa na ndege zisizo na rubani za kujitoa mhanga.
Uwanja wa ndege pekee unaofanya kazi nchini Sudan pia uliharibiwa, kusimamisha safari za ndege na kutatiza usafirishaji wa misaada muhimu.
Pengine shambulio lililoharibu zaidi lilikuwa ni la kituo cha umeme cha jiji hilo, ambalo uliiingiza Bandari ya Sudan gizani.
Hospitali zilipata shida kuendelea kufanya kazi kutokana na kupungua kwa akiba ya mafuta, wakati wakazi katika mikoa mingine inayoshikiliwa na jeshi tayari wameamua kuteka maji moja kwa moja kutoka Mto Nile au baharini kutokana na kuharibika kwa pampu za kupeleka maji majumbani.
Mashambulizi haya si ujanja wa kijeshi tu, ni sawa na hujuma za kiuchumi na kibinadamu.
Bandari ya Sudan ni msingi wa vifaa kwa misafara ya misaada ya Umoja wa Mataifa na usambazaji wa misaada.
Usumbufu wake unahatarisha kuongezeka kwa njaa na magonjwa katika nchi ambayo tayari inakabiliwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu ulimwenguni. Umoja wa Mataifa umeuita mji huo kama "njia pakee ya maisha", na RSF sasa inaikata.
Uharibifu wa mazingira na kikanda
Mbali na mateso inayokumba wanadamu, shida ya utulivu inajitokeza.
Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye vituo vya kuhifadhi mafuta yamezua moto unaoonekana kutoka maili kadhaa.
Kuonekana kwa moto kubwa kwenye ghala za mafuta huleta hofu ya uchafuzi wa sumu na uharibifu wa mazingira wa muda mrefu.
Katika Bandari ya Sudan, anga imegeuka kuwa jekundu kutokana na moto unaolishwa na mafuta sio tu ni athari ya kuona bali ni ya kimazingira, ambayo inazidisha hali ya hewa kwa wakazi.
Zaidi ya hayo, vituo vya kusafisha mafuta viko kwenye ufuo wa Bahari Nyekundu, na uharibifu wowote mkubwa unaweza kutoa mafuta machafu baharini, na kuhatarisha mifumo ya ikolojia ya baharini na maisha ya pwani.
Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye Bandari ya Sudan haya athiri tu nchi hiyo na yamezitia wasiwasi mataifa yenye nguvu za kikanda, zikiwemo nchi jirani za Saudi Arabia na Misri.
Cairo na Riyadh zote mbili zililaani mashambulizi hayo kwa haraka, zikihofia kwamba machafuko kwenye eneo la bahari nyekundu yanaweza kutishia njia za meli na kusababisha vurugu kwenye mipaka.
Matumizi ya ndege zisizo na rubani za hali ya juu na kundi lisilo la serikali huibua maswali ya dharura kuhusu ufadhili wa kigeni.
Kwa ufafanuzi zaidi, shambulio hilo linafanya vita vya Sudan kuwa vya kimataifa, na hivyo kusababisha hofu kwamba wahusika wa nje wanaweza kuzidisha ushiriki wao kulinda maslahi yao.
Serikali ya Sudan inailaumu Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ikiishutumu kwa kuipatia RSF teknolojia ya ndege zisizo na rubani, shitaka ambalo Abu Dhabi inakanusha vikali.
Kwa madai hayo, Sudan ilikata uhusiano wa kidiplomasia na UAE, baadaye kwa kiasi kidogo Sudan ilirudisha uhusiano huo; hii inaakisi hali halisi ya utegemezi wa kina wa Sudan kwa UAE kama kitovu cha mauzo ya dhahabu, biashara, miunganisho ya kifedha, na uhamishaji wa pesa kwa watu wake wengi wanaoishi nje ya nchi.
Bado, mashtaka hayo yanavunja juhudi za upatanishi wa kimataifa na inaleta hali tete zaidi katika mzozo huo.
Kutumwa kwa mifumo ya hali ya juu ya ndege zisizo na rubani pia kunaashiria mabadiliko muhimu katika vita vya kikanda, kufichua jinsi wanamgambo wasio wa serikali sasa wanapata teknolojia zilizokuwa zimehifadhiwa kwa wanajeshi wa kitaifa.
Matukio haya yanaibua wasiwasi mkubwa kuhusu utiririshaji wa silaha ambazo hazijadhibitiwa na urahisi wa silaha za kisasa kuvuka mipaka, mara nyingi kwa msaada wa mamlaka za kikanda zinazofuata ajenda zao wenyewe.
Matokeo yake ni enzi mpya ya mzozo wa wakala, ambapo wahusika wa nje wanaweza kuchagiza vita vya wenyewe kwa wenyewe kutoka mbali, kuzidisha ghasia, kudhoofisha mamlaka ya serikali, na kutatiza misaada ya kibinadamu.
Uzoefu huu unasisitiza hitaji la dharura la tahadhari ya kimataifa kwa uenezaji wa ndege zisizo na rubani na athari ya kudhoofisha nchi kupitia mienendo ya wakala katika migogoro ya kisasa.
Kuharibu uchumi
Mashambulizi hayo pia yanahatarisha njia ya kiuchumi ya Sudan Kusini. Kama taifa lisilo na bahari, inategemea kabisa mabomba ya Sudan na Bandari ya Sudan kusafirisha mafuta.
Mashambulio ya hivi majuzi ya ndege zisizo na rubani kwenye kituo kikuu cha kusukuma maji na tovuti ya kuhifadhi yanatishia kusitisha mtiririko huu.
Kusitishwa kunaweza kuharibu uchumi wa Juba ambao tayari ulikuwa dhaifu na kukata mapato muhimu kwa Sudan.
Mkataba wa usafirishaji wa mafuta wa Sudan na Sudan Kusini-unaotarajiwa kufanywa upya mwaka 2026, umeimarisha ushirikiano baada ya kujitenga na Sudan. Mashambulizi haya ya hivi punde yanahatarisha kutengua mpangilio huo maridadi na kuzivuta nchi zote mbili kwenye hali ya kutokuwa na utulivu zaidi.
Kilichoanza kama vita kwa ajili ya mji mkuu kimebadilika na kuwa vita dhidi ya njia za maisha za taifa - mzozo ambapo matangi ya mafuta, vituo vya umeme na shughuli za bandari sasa imegeuka kuwa michezo ya kulipizana kisasi.
Ongezeko hili linabeba gharama kubwa za kibinadamu: kwa kukandamiza upatikanaji wa nishati na misaada kwa Sudan, kunahatarisha kuitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi kubwa zaidi la mateso na kuigeuza nchi hio kuwa nchi iliyofeli.
Hali hiyo inahitaji hatua za haraka katika nyanja nyingi. Wahusika wa kimataifa lazima waingilie kati kidiplomasia kushinikiza kusitishwa kwa mapigano na kurejea kwenye mazungumzo, kusitisha uhasama ndio njia pekee ya kukomesha hali hii mbaya.
Mataifa yenye nguvu za kikanda kama vile Misri, Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Afrika yanapaswa kuzidisha shinikizo kwa RSF kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia na kuzishambulia njia za misaada ya kibinadamu.
Pia kuna haja ya kuwa na msukumo wa pamoja kulinda miundombinu muhimu: RSF inapaswa kuonywa vikali na jumuiya ya kimataifa kwamba mashambulizi ya makusudi kwenye vituo muhimu kwa maisha ya raia, kama vile gridi za umeme, bandari, maji, na usambazaji wa mafuta, ni uhalifu wa kivita chini ya sheria ya kimataifa.
Iwapo hiyo inamaanisha kutafura njia mbadala, kubadilisha maeneo ya usambazaji, au kutafuta usitishaji wa mapigano wa muda kwa ajili ya utoaji wa misaada, hatua ya haraka inahitajika.
Mataifa wafadhili yanapaswa kushughulikia mzozo wa Sudan kwa udharura unaostahiki, kuongeza ufadhili ili kuepusha njaa, kwani upunguzaji mkubwa wa misaada ya kimataifa ikiwa ni pamoja na upunguzaji mkubwa wa Marekani, umeacha shughuli za kibinadamu katika hatari kubwa.
Vita vya ndege zisizo na rubani za RSF haviharibu miundombinu ya Sudan; bali vinakata miunganisho ya mwisho ya nchi ya kuweza kuishi, utaratibu, na matumaini.
Jumuiya ya kimataifa lazima ichukue hatua za dharura: kushinikiza kusitishwa kwa mapigano, kulinda miundombinu muhimu ya kiraia, na kuhamasisha uingizaji wa misaada ya kibinadamu kwa kiwango kikubwa.
Ikiwa hayo hayatowezakana, ulimwengu unaweza kuhatarisha kuhalalisha aina mpya ya vita, ambayo njia za maisha inagekua kuwa shabaha, na mateso ya raia sio maafa tena, lakini mkakati wa kivita.
Lazima kuwe na kuwe na ufafanuzi kati ya kushambulia maisha ya raia na mkakati wa vita, kabla ya ndege zisizo na rubani kumaliza kile kilichosalia Sudan.
Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi si lazima yaakisi maoni na sera za uhariri za TRT Afrika.