AFRIKA
2 dk kusoma
Rais wa Zambia Hichilema asitisha maombolezo ya kitaifa ya Lungu
Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amefutilia mbali mpango wa kitaifa wa maombolezo ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Edgar Lungu baada ya mvutano na familia ya Lungu kuhusu mipango ya mazishi yake.
Rais wa Zambia Hichilema asitisha maombolezo ya kitaifa ya Lungu
Lungu alifariki katika mji mkuu wa Afrika Kusini Pretoria mnamo Juni 5, 2025/ picha: Reuters
20 Juni 2025

Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amefutilia mbali mpango wa kitaifa wa maombolezo ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Edgar Lungu.

Lungu, aliwahi kuwa rais wa sita wa Zambia kuanzia 2015 hadi 2021.

Kipindi cha maombolezo ya kitaifa, hapo awali kilianza Juni 8 hadi 14, na baadaye kiliongezwa kwa siku tisa, kutoka Juni 15 hadi 23.

Kuongezwa kwa muda huo kulikuja kufuatia mkutano wa hivi majuzi kati ya maafisa wa serikali na familia ya Lungu kutatua mzozo juu ya mpango wa mazishi yake.

Lungu alifariki Pretoria, Afrika Kusini Juni 5, 2025 akiwa na umri wa miaka 68. Alikuwa akitibiwa maradhi ambayo hayakutajwa.

Familia ya Lungu inaishutumu serikali kwa kukiuka makubaliano

Baada ya serikali na familia ya Lungu kukubaliana hivi majuzi juu ya mpango wa mazishi, mwili wa rais huyo wa zamani ulipaswa kurejeshwa nchini Zambia Jumatano, Juni 18 kabla ya kuagwa na wananchi kwa siku tatu katika mji mkuu wa Lusaka, ibada ya mazishi Jumapili na mazishi Jumatatu, Juni 23.

Hata hivyo familia ya Lungu ilizungumza na waandishi wa habari Jumatano, ikisema kuwa serikali ilipuuza makubaliano yake kuhusu mipango ya mazishi, hivyo basi kufuta mpango uliopangwa wa kurejea nyumbani na kuzikwa baadaye.

Familia ya Rais wa zamani wa Zambia Edgar Lungu ilichelewesha kurejeshwa kwa mwili wake kutoka Afrika Kusini kwa mara ya pili Jumatano katika mzozo na kiongozi wa sasa wa nchi hiyo kuhusu maelezo ya mazishi.

Wakili wa familia hiyo alisema kuwa hawataleta mwili wa Lungu nyumbani kama ilivyopangwa Jumatano kwa sababu hawataki Rais Hakainde Hichilema ahudhurie mazishi ya Lungu.

Lungu na Hichilema walikuwa wapinzani wakubwa kisiasa.

Katika hotuba yake siku ya Alhamisi, Rais Hichilema alisema Lungu, akiwa rais wa zamani, "ni wa taifa la Zambia" na mabaki yake kwa hiyo "yanapaswa "kuzikwa nchini Zambia kwa heshima kamili, na si katika taifa lingine lolote."

Zambia 'haiwezi kumudu hali ya maombolezo ya muda usiojulikana'

Wakati akitangaza kusitishwa kwa programu ya maombolezo ya kitaifa iliyoongezwa muda rais alisema, "nchi yetu haiwezi kumudu hali ya maombolezo ya muda usiojulikana. Tumefanya kila tuwezalo kushirikisha familia ya rais wetu wa sita wa jamhuri aliyeaga dunia. Na tumefikia tunapoweza.”

"Kutokana na mazingira hayo, napenda kuliarifu taifa kuwa hadi kufikia mwisho wa leo Juni 19, 2025, kipindi hiki mahususi cha maombolezo ya kitaifa kimekwisha rasmi. Hii itaiwezesha nchi kuanza kurejea katika hali ya kawaida,” amesema Rais.

Wanafamilia wa Lungu, akiwemo mjane wake Esther Lungu, kwa sasa wana kesi mahakamani zinazohusiana na ufisadi.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us