Idadi ya waliolazimika kuhama makazi yao kutokana na vita, machafuko na mateso imefikia milioni 122.1 kote duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya wakimbizi (UNHCR) limesema Alhamisi, wakiitaja hali hii kuwa “iliyo mbaya sana.”
Kulingana na ripoti ya UNHCR kuhusu yanayoendelea duniani, idadi ya waliohama makazi yao imeongezeka kutoka milioni 120 mwaka jana, kutokana na mapigano ya muongo mmoja kwa ujumla katika nchi za Sudan, Myanmar, Ukraine, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na maeneo mengine.
"Idadi ya watu walioondolewa katika makazi yao na vita, machafuko na mateso duniani imekuwa mbaya sana, hasa kipindi ambacho misaada inapungua," shirika hilo limesema. "Sehemu ambayo kuna mafanikio kidogo ni pale ambapo watu wanarejea kwao, hasa nchini Syria."
Sasa hivi nchini Sudan inakabiliwa na janga baya zaidi la watu kuondolewa katika makazi yao, watu milioni 14.3 wameondolewa katika maeneo yao, ikiwa ni zaidi ya Syria ambayo watu wake walioondolewa katika makazi yao ni milioni 13.5, Afghanistan milioni 10.3 na Ukraine milioni 8.8, ripoti hiyo imesema.
'Hali ya usalama ni tete'
"Tunaishi kipindi ambacho hali ni tete sana ... huku watu wengi wakipitia madhila. Lazima tufanye juhudi zaidi za kutafuta amani na suluhu ya kudumu,” Alisema Kamishna wa masuala ya wakimbizi wa Umoja wa Mataifa Filippo Grandi.
Wakimbizi wa ndani ya nchi walikuwa milioni 73.5 kufikia mwishoni mwa 2024, huku wakimbizi walioko nje ya nchi wakiwa milioni 42.7.
Licha ya kupungua kwa ufadhili tangu 2015, ripoti inaonesha kuwa watu milioni 9.8 walirudi nyumbani 2024, ikiwemo wakimbizi milioni 1.6 — idadi kubwa zaidi katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili — na milioni 8.2 walikuwa wakimbizi wa ndani.
Raia wa Syria wamerudi nyumbani
"Karibu Wasyria milioni mbili wamefanikiwa kurudi kwao baada ya kuondolewa kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita," Grandi alisema, akitoa onyo kuwa wanarejea katika mazingira ambayo ni tete sana.
Shirika la UNHCR limetoa wito wa ufadhili kutolewa ili kuwasaidia wale wanaorudi nyumbani, jamii zinazowapokea, na miradi ya misaada iliyo muhimu kwa usalama na ustawi wa nchi.