Mahakama nchini Kenya Alhamisi imewapa wachunguzi siku 15 kukamilisha uchunguzi wao wa maafisa wawili wanaoshukiwa kumpiga risasi na kumjeruhi muuza barakoa wakati wa maandamano ya hivi majuzi ya kupinga mauaji ya mwanablogu aliyefariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Maafisa hao walifikishwa mahakamani siku mbili baada ya kufyatua risasi wakati wa maandamano huku kamera zikinasa tukio hilo. Ilisababisha hasira na malalamiko zaidi kuhusu ukatili wa polisi.
Maandamano ya Jumanne katika mji mkuu yamekuja baada ya hali ya taharuki kuzuka juu ya kifo cha mwanablogu, Albert Ojwang, ambaye alipatikana amefariki akiwa katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi.
Ojwang alikamatwa 6 Juni magharibi mwa Kenya kwa kile polisi walichosema kuandika “taarifa za uwongo” kuhusu afisa mmoja mwandamizi wa polisi katika mitandao ya kijamii. Polisi walidai kuwa kifo chake ni kutokana na “kujigonga kwenye ukuta wa kituo hicho,” lakini wanaharakati walitilia shaka chanzo cha kifo chake.
Kuachia ngazi
Siku ya Jumanne waandamanaji walitaka naibu inspekta jenerali wa polisi, Eliud Lagat, ambaye aliwasilisha malalamiko ya kuharibiwa sifa dhidi ya Ojwang, akamatwe.
Lagat alisema Jumatatu kuwa anaachia ngazi na atashirikiana na wachunguzi. Maafisa hao wawili wa Kituo cha Polisi cha Central walikamatwa wiki iliopita.
Maafisa hao watabaki kizuizini hadi 3 Julai. Wakati walipofikishwa mahakamani walificha nyuso zao na barakoa, na kuzua malalamiko kutoka kwa wanaharakati.
Kenya ina historia ya ukatili wa polisi, na Rais William Ruto amewahi kusema kuwa atamaliza ukatili huo, pamoja na kuuawa kwa watu kiholela.
Mwaka uliopita, wanaharakati kadhaa na waandamanaji walitekwa na kuuawa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga ongezeko la kodi. Maandamano hayo pia yalikuwa na wito wa kumtaka Ruto aondoke madarakani.