Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Mahamoud Ali Youssouf, ameeleza wasi wasi wake mkubwa kufuatia ripoti za mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Iran na kuendelea kwa uhasama katika eneo la Mashariki ya Kati.
Israeli ilifanya mashambulizi makubwa ya anga yaliyolenga mji mkuu wa Iran, Tehran na miji mingine kote nchini humo kuamikia Ijumaa.
“Mwenyekiti anatoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa uhasama na kuwataka wahusika wote kujizuia kutumia nguvu,” taarifa kutoka Tume ya Umoja wa Afrika imesema.
Youssouf amesema kuwa matukio ya sasa yanatishia sana amani na usalama wa kimataifa.
“Umoja wa Afrika unasisitiza dhamira yake thabiti ya amani, mazungumzo na utatuzi wa amani wa migogoro,” taarifa ya Mwenyekiti wa Tume hiyo ya kibara imeongezea.