Serikali ya Kenya imeongeza hatua yake ya kukabiliana na ugonjwa wa kala-azar unaokumba kaunti ya kaskazini-mashariki mwa Wajir huku takwimu mpya zikionyesha kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa huo imefikia 25.
Kala azar ni home isiyo ya kawaida, inayochangia kupoteza uzito na anemia. Isipotibiwa mapema inaweza kusababisha vifo kwa zaidi ya asilimia 95 ya maambukizi.
Kala azar husababishwa na kuumwa na nzi wa kike aina ya “sandfly.”
Wizara ya Afya inasema mambukizi yanaonekana kuongezeka hadi kwa zaidi ya watu 600, wengi walioathirika wakiwa watoto.
Takwimu mpya zinaonyesha kuwa watu 106 wanapokea matibabu katika vituo mbali mbali katika kaunti ya Wajir, iliyoathiriwa zaidi ni hospitali ya kaunti ya level 4 ambapo shughuli nyingi zimehamishwa.
Akiongea Ijumaa asubuhi alipozindua maabara zinazohamishika katika kaunti ya kaskazini mashariki ili kusaidia utambuzi wa mapema, viwango vya afya ya umma na taaluma, Katibu Mkuu wa Wizra ya Afya, Mary Muthoni anasema serikali, kupitia Hazina ya Kitaifa itatoa pesa za kusaidia kukabiliana na ugonjwa huo ambao hadi sasa umesababisha vifo zaidi ya 20 tangu kuzuka kwa ugonjwa huo Septemba 2024.
Kaunti ya Wajir imekiri kulemewa na maambukizi.
Maabara zinazohamishika zitasaidia sana katika kuimarisha utambuzi wa mapema kwani wagonjwa wengi walikuwa wakipelekwa kwenye vituo vya afya wakiwa tayari wamezidiwa.
Katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo, nchini Kenya Shirika la Afya Duniani, WHO kupitia Kituo chake cha dharura cha Nairobi, limetoa vifaa muhimu vya matibabu.
Hivyo ni pamoja na vipimo vya haraka vya uchunguzi ili kuchunguza angalau watu 250, na vifaa vyengine kusaidia katika kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, uchunguzi, na matibabu kwa wakati.
“Kala-azar hupatikana katika Baringo, Pokot Magharibi, Turkana, Marsabit, Isiolo, Garissa, Wajir, Mandera, Kitui, Tharaka Nithi, na Kajiado. Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na mienendo ya watu, magonjwa haya yanaenea katika maeneo mapya,” Shirika la AMREF limesema.