AFRIKA
2 dk kusoma
Viongozi mbalimbali watuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Zambia
Itakumbukwa pia kuwa, kiongozi huyo mstaafu wa Zambia aliwahi kufutiwa mafao yake ya kustaafu kutokana na nia yake yakutaka kugombea tena urais katika uchaguzi wa mwaka 2026.
Viongozi mbalimbali watuma salamu za rambirambi  kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Zambia
Rais Mstaafu wa Zambia, Edgar Changwa Lungu / TRT Afrika Swahili
6 Juni 2025

Viongozi mbalimbali kutoka Afrika na nje ya bara wametuma salamu zao za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa Zambia Edgar Changwa Lungu. Taarifa za kufariki kwa kiongozi huyo wa zamani wa Zambia zilitolewa Juni 5 na chama chake cha Patriotic Front, ambacho kilithitibisha kufariki kwa Lungu akiwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.

Miongoni mwa viongozi waliotuma salamu za rambirambi ni pamoja na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambae ameonyesha kusikitishwa na kifo cha Lungu aliyefariki akiwa na umri wa miaka 68.

Nae Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa pia ametuma salamu zake za rambirambi.

Kwa upande wake, Rais wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah amempongeza Lungu kwa kudumisha uhusiano kati ya nchi mbili hizo.

Rais wa Kenya William Ruto, amesifu uliokuwa uongozi wa Lungu na kusema, “Rais Lungu alikuwa ni kiongozi wa aina yake na mleta maendeleo aliyetumikia raia wa Zambia kwa nguvu na kujitolea.”

Chama cha upinzani cha Afrika Kusini cha Economic Freedom Fighters (EFF) kimemsifu Lungu kwa kuanzisha sera ambazo zimepanua wigo wa uchumi wa Zambia pasina kutegemea madini ya nchi hiyo na kuunga mkono ukuaji wa miundombinu.

Moise Katumbi, ambae ni kiongozi wa upinzani kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amesema, “Rais Lungu alikuwa mtu muhimu, ambae wakati akiwa madarakani, alitetea amani katika kanda nzima na siku zote aliiweka DRC moyoni mwake.”

Lungu alikuwa rais wa Zambia kati ya mwaka 2015 hadi 2021, aliposhindwa katika uchaguzi na rais aliye madarakani Hakainde Hichilema.

Kufuatia nia yake ya kutaka kurudi tena katika siasa kwa lengo la kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2026, ikiwemo kugombea urais kwa sababu, kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, tayari alikuwa amemaliza muda wake.

Itakumbukwa pia kuwa, kiongozi huyo mstaafu wa Zambia aliwahi kufutiwa mafao yake ya kustaafu kutokana na nia yake yakutaka kugombea tena urais katika uchaguzi wa mwaka 2026.

Kwa mujibu wa serikali ya nchi hiyo, sheria inasema kwamba, rais mstaafu akitaka kurudi katika siasa, sharti aachie mafao yao.

Katika taarifa rasmi, Rais Hakainde Hichilema ameelezea kusikitishwa kwake kwa niaba ya taifa, na kutoa salamu zake za rambirambi kwa mke wa marehemu Esther Lungu, familia yake, chama cha Patriotic Front na watu wote, huku akisema kuwa, kifo cha Lungu ni msiba mkubwa kw taifa.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us