Kama ilivyo katika michezo mbali mbali huwa kuna ukomo au pengine kustaafu kwa mchezaji. Katika mchezo wa mpira wa kikapu pia wachezaji hufikia kipindi wakaamua kuondoka mchezoni.
Sababu zinaweza kuwa nyingi, kwa wengine ni umri kuwa mkubwa kushindwa kuhimili tena mikiki mikiki kama enzi za ujana, wengine ni majeraha, au wengine ni maamuzi tu.
Hebu tuangalie baadhi ya wachezaji ambao walikuwa kwenye ligi ya NBA, tupate kufahamu wako wapi sasa hivi.
LUOL DENG
Luol Ajou Deng alizaliwa Sudan miaka 39 iliyopita, na ana uraia pacha wa Sudan Kusini na Uingereza. Alianza kucheza katika ligi ya NBA mwaka 2004 akiwa na timu ya Phoenix Suns.
Alicheza pia katika timu za Chicago Bulls, Miami Heat, Los Angeles Lakers na Minnesots Timberwolves. Deng mwenye urefu wa futi 6 na inchi 9 alistaafu na kuanzia 2019 amekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu la Sudan Kusini.
Pia hujishughulisha na masuala ya kuwasaida wakimbizi.
HASHEEM THABEET
Ni raia wa Tanzania mwenye urefu wa futi 7 na inchi 3. Alianza kucheza mpira wa kikapu akiwa na umri wa miaka 15. Mwaka 2009 alikuwa mchezaji wa kwanza aliyezaliwa Tanzania kucheza katika ligi ya NBA, kipindi hicho akijiunga na timu ya Memphis Grizzlies.
Alicheza pia katika timu za Houston Rockets, Portland Trail Blazers na Oklahoma City Thunder. Thabeet mwenye umri wa miaka 37 pia alicheza katika ligi ya nje ya Marekani
na kufikia mwaka 2024 alikuwa amejiunga na timu ya nyumbani Tanzania Dar City na aliisaidia timu hiyo kupata mafanikio waliposhiriki mashindano ya kwanza ya mpira wa kikapu kwa timu za Afrika Mashariki.
DJ MBENGA
Didier ‘’D.J’’ Ilunga-Mbenga alizaliwa Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka 1980. Ana uraia pacha wa DRC na Ubelgiji.
Uhodari wake wa kucheza mpira wa kikapu ulionekana wakati alipokuwa anaishi Ubelgiji. Alipata fursa ya kucheza kwenye ligi kuu ya nchini humo akiwa na timu tofauti.
Alianza kucheza kwenye ligi ya NBA mwaka 2004. Mbenga mwenye urefu wa futi 7 kamili alikuwa katika timu za Dallas Mavericks, Golden State Warriors, Los Angeles Lakers na New Orleans Hornets.
Pia aliwahi kucheza katika ligi ya Ufilipino. Mwaka 2005 alianzisha wakfu wa Mbenga kwa lengo la kuwasaidia watoto nchini DRC pamoja na kuwapa usaidizi wakimbizi nchini Ubelgiji.
Safari ni hatua, wamevuma wakiwa kwenye ligi kubwa ya mpira wa kikapu duniani na wanaendelea kuvuma katika safari zao nyingine za maisha.