Ni wakati mwengine ambapo Uganda inakaribisha mahujaji kutoka sehemu tofauti nchini mwake na nchi nyengine barani na kimataifa.
Kila Juni 3, waumini wa Kanisa Katoliki na Waprotestanti hukutana katika Madhabahu ya Namugongo, maarufu Uganda Martyrs Shrine Namugongo.
Ipo takriban kilomita 15 kutoka mji mkuu wa Kampala.
Hili ni mojawapo ya maeneo makubwa zaidi ya Hija ya Kikristo barani Afrika yaliyowekwa kwa ajili ya kuwakumbuka Waanglikana 23 na wengine 22 wa Kikatoliki ambao waliuawa kati ya 1885 na 1887 kwa amri ya mfalme wa Buganda, Kabaka Mwanga II.
Mahujaji wengi huamua kutembea kutoka maeneo yao hadi Namugongo. Kwa mfano hawa walikuwa wa kwanza kuwasili 24 Mei, baada ya kutembea zaidi ya kilomita 370. Hawa kutoka Kenya nao walivuka mpaka kwa miguu.
Wanaotembea husimama katika vituo tofauti, na kupeana moyo kwa kuimba na maombi.Baadhi ya mahujaji walieleza kwamba safari yao pia ni sala ya amani, umoja, uponyaji wa ndani, na ukombozi wa familia.
Tanzania ni kati ya nchi ambazo huwa na mahujai wengi pia kila mwaka. Misa maalumu ilifanywa tarehe mosi Juni, ili kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania aliyefariki dunia 1999.
Tamaduni ya maombi haya ilianzishwa baada ya Papa Benedict XVI kumtangaza Nyerere kuwa mtumishi wa Mungu mnamo Mei 13, 2005, ikiwa ni hatua ya kwanza kuelekea kutangazwa kwake kuwa mwenye heri na kutawazwa kuwa mtakatifu.
Kwa mahujaji ambao huamua kupitia changamoto ili kufika hapa kila mwaka, kuja Namugongo siyo sherehe ya kidini tu bali ni wakati wa ukumbusho wa pamoja kusherehekea wale waliosimama kwa ajili ya ukweli na dhamiri licha ya mateso.
Misa ambayo hufanywa Juni 3 huwa ndio kilele cha sherehe hizi. Sherehe za 2024 zinakadiriwa ziliwavutia takriban mahujaji 689,637 wa ndani ya nchi na nje. Huku eneo la maombi ya wakatoliki likikadiriwa kuwa na mahujaji 563,940 na Kanisa la Kiprotestanti, 125,697.
Serikali inatazamia kuwa idadi ya watu mwaka huu itakuwa juu zaidi.